Jumatano tarehe 19 Juni, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 12 Dhulhija 1445 Hijria sawa na tarehe 19 Juni 2024.
Siku kama ya leo miaka 972 iliyopita alizaliwa Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran.
Akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusoma elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kutunga mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika tungaji wa mashairi.
Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho ndani yake ameeleza wazi fikra zakke za kiakhlaqi na irfani. Vitabu vingine mashuhuri vya malenga huyo ni 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq".
Miaka 505 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 12 Dhul-Hijja mwaka 940 Hijria, aliaga dunia Ali bin Hassan Karaki Amili mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu.
Alipata elimu ya msingi katika eneo alikozaliwa la Jabal Amil nchini Lebanon. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Ali bin Hassan Karaki alifanya safari katika nchi kdhaa za Kiislamu. Mhakiki Karaki kama anavyojulikana zaidi, ameacha athari nyingi za vitabu zenye thamani kubwa. Jamiul Maqaasid na Risatul Adalah ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.
Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Baada ya Benito Juarez kupata urais wa Mexico mwaka 1855, aliwang'anyya mamlaka wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini humo. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa ambao walituma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji wazungu. Hata hivyo, Juarez aliendeleza mapambano dhidi ya majeshi ya Ufaransa na washirika wake, na baada ya kuwashinda na kumnonga mfalme wa kutwishwa, akashika tena urais wa Mexico.
Katika siku kama ya leo miaka 147 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1877, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri.
Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu wa Kipolandi, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait.
Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita magaidi wa kundi la MKO walitenda jinai kubwa ya kutisha katika Haram tukufu ya Imam Ridha (a.s), mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) katika mji mtakatifu wa Mash'had.
Bomu liliripuka ndani ya haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) alasiri ya siku ya Ashura mwaka huo wakati watu walipokuwa wakifanya ziara na marasimu ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s). Makumi ya waumini na wapenzi wa Ahlul Bait (a.s) waliuliwa shahidi au kujeruhiwa katika haram hiyo. Mlipuko huo ulisababisha hasara na maafa mengi katika haram hiyo tukufu.
Na katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia alifariki dunia Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, mlinganiaji mkubwa wa Uislamu katika kanda ya Mashariki mwa Afrika.
Hujjatul Islam Walmuslimin Rizvi alizaliwa huko mashariki mwa India na baada ya kupata masomo ya awali kwa baba yake alijifunza masomo ya juu na lugha za Kingereza, Kiarabu, Kifarsi na Urdu na kupata daraja ya Fakhrur Afadhil. Baada ya kulingania dini kwa miaka mingi nchini India, Sayyid Akhtar Rizvi alihisi wajibu wa kuelekea Tanzania, barani Afrika, na kuanza kueneza maarifa ya dini na mafundisho ya Ahlubaiti wa Mtume (saw).
Allamah Rizvi ameandika na kufasiri vitabu vingi kwa lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafsiri ya Qur'ani ya al Miizan na kitabu cha Al Ghadir na kujenga makumi ya misikiti, madrasa, maktaba na zahanati. Alifariki dunia jijini Dar es Salaam katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 20 Juni mwaka 2002 kwa mwaka wa Miladia akiwa na umri wa miaka 75.