Hikma za Nahjul Balagha (54)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 54 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 54 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 47.
قَدْرُ الرَّجُلِ عَلَى قَدْرِ هِمَّتِهِ، وَ صِدْقُهُ عَلَى قَدْرِ مُرُوءَتِهِ، وَ شَجَاعَتُهُ عَلَى قَدْرِ أَنَفَتِهِ، وَ عِفَّتُهُ عَلَى قَدْرِ غَیْرَتِهِ
Thamani ya mtu inategemea hima yake na ukweli wake unategemea shakhsia yake na ushujaa wake unategemea uzuhdi wake na staha yake inategemea ghera yake.
Katika hikma hii ya 47 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS kwa mara nyingine tena anatoa miongozo minne ambayo yenyewe nayo ni chimbuko na ni asili ya kanuni nyingine nne. Anasema: Thamani ya mtu inategemea hima yake na ukweli wake unategemea shakhsia yake, na ushujaa wake unategemea uzuhdi wake (yaani kutopumbazwa na kutojifunga na masuala ya kimaada na ya kidunia) na staha yake inategemea ghera yake ya moyoni.
Kwa kawaida, baadhi ya watu hutafuta furaha nje ya dhati yao, bila ya kujua kwamba furaha ya kweli inatokana na wao wenyewe. Matendo yake mtu yana taathira za moja kwa moja kwake yeye mwenyewe kabla ya kumfikia mtu mwingine. Kwa bidii na uvumilivu, mtu anaweza kujijengea hatima nzuri yeye mwenyewe.
Hima ni ule uamuzi ambao mtu mwenyewe huuchukua kwa ajili ya kufanikisha mambo muhimu. Kadiri maamuzi yake hayo yanavyokuwa makubwa na kadiri bidii yake inavyoongezeka, ndivyo mafanikio yake yanavyokuwa makubwa zaidi. Hima ziko za namna nyingi. Baadhi ya watu hima yao kuu ni kumiliki mali na wanaelekeza tamaa zao zote huko bila ya kujua kuwa, tamaa na hima ya namna hiyo isiyojali kitu kingine isipokuwa mali, utajiri na mambo ya kimaada; ni hima chapwa isiyo na mwisho mwema. Wengine hima yao kuu ni kulea familia zao kwa njia sahihi, hima za wengine ni kurekebisha tabia za watu waliowazunguka na wengine hima yao ni kutaka kurekebisha mji mzima, mikoa na wilaya zake. Wengine ni kutaka kuitawala dunia kwa hali yoyote iwayo. Hima ya wengine lakini ni kuziletea maendeleo jamii zao, maendeleo ya kisayansi, kiteknolojia na kiroho. Kiujumla hima ziko za aina nyingi. Ni kwa sababu hii ndio maana hapa Imam Ali AS anasema: Thamani ya kila mtu inategemea hima yake.
Kama tunavyojua vyema pia kwamba, kila kitu kina kipimo chake na kila kitu kinapimwa na chombo maalumu kinachonasibiana nacho. Kwa mfano vitu vya majimaji, kipimo chake ni lita. Vitu vigumuvigumu kawaida hupimwa kwa kilo. Hewa nayo ina kipimo chake maalumu, bali kila kitu kinapimwa kwa chombo kinachooana nacho. Ni hivyo hivyo, kipimo cha imani na uungawana wa mtu ni ukweli na uaminifu wake. Kwa kweli ni sifa hiyo ya ukweli na uaminifu ndiyo huainisha shakhsia ya mtu na hadhi yake. Mtu mwenye heshima na shakhsia nzuri, huchukia kusema uongo. Mara nyingi imetokezea uongo wa mtu ukafichuka na kumuumbua aliyeusema. Ndio maana mtu mwenye heshima zake hujitahidi mno kuwa mbali na mambo ya uongo. Ndio maana pia kwamba, katika sehemu ya pili ya Hikma ya 47 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anasema, shakhsia na uungwana wa kila mtu kipimo chake ni ukweli na uaminifu wake.
Msingi mkuu mwingine wa tatu uliotajwa na Imam Ali AS katika hikma hii ya 47 ni ushujaa ambao chimbuko lake hasa ni kupinga uhalifu na mambo maovu. Ni wazi kwamba wakati mtu anapotilia hima tu masuala ya jaha, cheo na mali pamoja na hawaa na matamanio ya nafsi, ushujaa wake hupungua na baadaye huwa mateka na mtumwa wa hawaa za nafsi yake. Lakini wakati anapojikomboa kutoka kwenye minyororo hiyo, ushujaa wake huongezeka na huwa tayari kutetea haki na kufuata njia sahihi bila ya kuogopa kupoteza matamanio ya kupita na ya kupumbuza ya kiduia. Imam Ali anatufundisha hapa akisema, ushujaa wa kila mtu unategemea uzuhdi na kutokubali kwake kutekwa na mambo ya kidunia.
Amma katika sehemu ya nne na ya mwisho ya hikma hii, Imam Ali AS anasema, staha ya mtu inategemea ghera yake. Neno 'iffa hapa ni kwa maana ya kujizuia na kuchukia mtu kuangalia mambo maovu na ghera hapa ni kwa maana ya kulinda thamani na matukufu yake na kuchunga kikamlifu haki zake za kibinadamu na majukumu yake mbele ya Muumba wake.
Ni dhahiri kwamba, mtu mwenye ghera na heshima yake, lazima atachunga heshima za wengine na ndio maana kadiri ghera ya mtu inapokuwa kubwa ndivyo staha na heshima yake nayo inavyozidi kuwa kubwa pia.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.