Hikma za Nahjul Balagha (70)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 70 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 70 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 62.
إِذَا حُیِّیتَ بِتَحِیَّة فَحَیِّ بِأَحْسَنَ مِنْهَا، وَإِذَا أُسْدِیَتْ إِلَیْکَ یَدٌ فَکَافِئْهَا بِمَا یُرْبِی عَلَیْهَا، وَالْفَضْلُ مَعَ ذَلِکَ لِلْبَادِی
Unapoamkiwa kwa maamkizi, jibu kwa maamkizi yaliyo bora zaidi, na unaponyooshewa mkono wa kupewa zawadi, lipa kwa zawadi bora zaidi na ubora wa fadhila ni wa yule anayetangulia kutenda jema.
Katika hikma hii ya 62 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anagusia msingi mwingine muhimu wa Qur’ani Tukufu na wa wa dini ya Kiislamu kwamba Muislamu anaposalimiwa, ni wajibu wake kurejesha salamu na imehimizwa mno kurejesha salamu kwa njia iliyo bora zaidi. Muislamu anapotendewa wema, hulipa wema huo kwa njia na namna bora zaidi. Zaidi ni kwamba fadhila bora zaidi huenda kwa yule anayetangulia yeye kuwafanyia wema watu wengine bila ya kusubiri sababu. Naam:
إِذَا حُیِّیتَ بِتَحِیَّة فَحَیِّ بِأَحْسَنَ مِنْهَا، وَإِذَا أُسْدِیَتْ إِلَیْکَ یَدٌ فَکَافِئْهَا بِمَا یُرْبِی عَلَیْهَا، وَالْفَضْلُ مَعَ ذَلِکَ لِلْبَادِی
Uislamu kwa maadili yake bora yasiyo na kifani unatufundisha kwamba, kila jambo jema lazima lijibiwe kwa jema bora zaidi haijalishi wema huo tumefanyiwa kwa maneno ya heshima au kwa kitendo chema, muhimu ni kwamba muungwana hakai na deni na anapofanyiwa wema hulipa kwa wema mkubwa zaidi. Kwa mfano mtu anapotutolea salamu ya kutuombea dua ya amani kwa kutwambia Assalaamu Alaykum, yaani amani iwe juu yako, kabla ya jambo lolote huwa ni wajibu kwetu kujibu salamu hiyo na inavyohimizwa zaidi na Uislamu ni kujibu kwa njia bora zaidi na kusema kwa mfano amani, baraka, usalama na rehema za Allah ziwe juu yako pia - Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tabia hiyo njema bila ya shaka yoyote huimarisha mahaba na udugu baina ya watu katika jamii na kufanya mapenzi ya kupenda kupigania haki na urafiki baina ya watu kuwa makubwa zaidi. Ni wazi kwamba maisha katika jamii kama hiyo huwa muda wote yamejaa utulivu na watu kusaidiana na kutokuwepo uadui kabisa baina yao kwani muda wote wanatakiana amani na usalama.
Viongozi wakubwa wa dini tukufu ya Kiislamu wametuonesha mifano mingi ya kivitendo ya maadili hayo bora ya Ki-Qur’ani. Zimepokewa hadithi nyingi zinazothibitisha jambo hilo. Miongoni mwake ni hii inayosema kwamba, siku moja tulikuwa tumekaa pamoja na Imam Hasan bin Ali AS. Mara akaingia kijakazi na kumpa zawadi ya ua Imam. Hapo hapo Imam Hasan AS alimwambia kuanzia hivi sasa wewe ni huru kwa kwa ajili ya Allah. أنْتِ حُرةُّ لِوَجْهِ اللّهِ تَعالى Sisi tuliokuwepo hapo tulimuuliza Imam, mbona umemwachilia huru kwa zawadi ya ua tu alilokupa wakati ua halilingani hata chembe na thamani yake? Imam alijibu kwa kusema: Hivi ndivyo alivyotulea kwa maadili bora Mola wetu Mtukufu. Baada ya hapo Imam alisoma aya ya 86 sura tukufu ya al Nisaa ambayo inasema: Na mnapoamkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhisabu kila kitu.
Amma swali linalojitokeza hapa ni nini hikma ya Imam Ali AS kusema hapa ubora wa fadhila anakuwa nao aliyetangulia kutenda wema? Majibu yake ni kwamba aliyetendewa wema huwa anachofanya ni kulipa fadhila baada ya kutendewa wema huo. Huenda asingelazimika kujibu kama asingetokea mtu wa kumtendea wema huo. Lakini yule aliyetangulia kutenda wema, huwa amefanya hivyo bila ya kutanguliwa na chochote. Amefanya kwa uungwana na kwa maadili yake bora na kamwe hakufanya hivyo kulipa fadhila.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Husain AS ambayo inasema: Maamkizi ya Kiislamu yana thawabu 70. 69 kati ya thawabu hizo zinakwenda kwa aliyetangulia kutoa salamu na moja huenda kwa anayejibu salamu.
Hadithi kama hiyo imepokewa pia kutoka kwa Imam Ali AS katika vitabu vya Hadithi cha Biharul Anwar na Mustadrak al Wasail.
Zaidi ya hayo ni kwamba mtu anayetangulia kutoa salamu, huwa amedhihirisha kwa uwazi pia maadili mengine bora nayo ni unyenyekevu na kutojiona bora mbele ya wengine. Ni kuonesha kutokuwa na kiburi mbele ya ndugu yake wa kidini, wakati anayejibu salamu na maamkizi hayo ya Kiislamu huwa anatekeleza wajibu wake wa kidini na kulipa fadhila
Ni vyema tuseme pia hapa kwamba neno usdiyat lililomo kwenye hikma hii ya 62 ya Nahjul Balagha lina maana ya kumnyooshea mtu mkono. Hivyo ibara inayosema Usdiyat ilayka yadun kwenye hikma hii mafhumu yake ni istiara yenye maana ya kupewa hidaya na zawadi.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.