Silaha za Australia zinatumika katika mauaji ya kimbari Sudan?
-
Darfur, Sudan
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), unaoshutumiwa kwa kuunga mkono waasi wa RSF wanaotekeleza ukatili na mauaji ya kimbari Sudan, umeibuka kuwa soko kubwa zaidi la silaha za Australia.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Australia imeiuzia UAE silaha zenye thamani ya takribani dola milioni 300.
Hivi sasa nchini Australia, wabunge, mashirika ya haki za binadamu na makundi ya kidini wanataka kusitishwa kwa mauzo ya vifaa vya ulinzi na silaha kwenda UAE, wakitaja ripoti za mara kwa mara za wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kwamba nchi hiyo ya Kiarabu imekuwa ikiwapatia silaha waasi wa RSF wanaoshutumiwa kwa mauaji ya kimbari.
Kundi hilo la linashutumiwa kwa kuendesha kampeni ya mauaji ya kimbari, ubakaji na mateso ambayo yameongezeka baada ya kutekwa kwa mji wa El Fasher mwezi uliopita, katika eneo la Darfur lililokumbwa na njaa.
Maelfu wanaripotiwa kuuawa na waasi wa RSF wakati wa kutekwa mji huo.
Ukubwa wa mauaji hayo umethibitishwa na picha za setilaiti zilizoonyesha miili ardhini na mabadiliko makubwa ya rangi ya udongo uliojaa wekundu na damu.
Kundi la RSF, ambalo awali lilikuwa mshirika wa serikali ya Sudan lakini sasa linapambana nayo, limepata “silaha za kisasa” kutoka UAE kupitia Chad na Libya. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa UN ambao wanasema RSF imetumia silaha hizo kuwaua watu wanaoiunga mkono serikali ya Sudan.
Ushahidi unaongezeka unaonesha kwamba UAE inaipatia RSF silaha na mkabala wake inapokea dhahabu. Inakadiriwa kuwa katika miaka ya hivi karibuni, asilimia 90 ya dhahabu ya Sudan, yenye thamani ya takribani dola bilioni 13.4 inatoroshwa kinyume cha sheria kutoka nchin hiyo ambapo sehemu kubwa hupelekwa UAE.
Kikosi cha wataalamu wa UN kilieleza mwezi Aprili kuhusu mzunguko mkubwa wa ndege za mizigo kutoka UAE, zikidaiwa kubeba silaha, risasi na vifaa vya matibabu kwa RSF kupitia Chad.
Jeshi la UAE lenyewe limewahi kushutumiwa kwa uhalifu wa kivita na kuvunja marufuku ya silaha huko Yemen na Libya.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, licha ya wasiwasi wa mashirika ya haki za binadamu, serikali ya Australia inaamini uhusiano wa kijeshi na UAE unaweza kupanuliwa zaidi. Australia inapuuza ukweli kwamba wataalamu wanaamini baadhi ya silaha hizo zinatumika kutekeleza mauaji ya kimbari Sudan tangu Aprili 2023 wakati vita vya sasa vilipoanza.