Hikma za Nahjul Balagha (57)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 57 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 57 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 50.
قُلُوبُ الرِّجَالِ وَحْشِیَّةٌ، فَمَنْ تَأَلَّفَهَا أَقْبَلَتْ عَلَیْه
Nyoyo za watu ni zenye shakashaka na woga, muda wote huelekea kwa anayezizoeza na kuzifanyia upole.
Katika hikma hii iliyojaa mafunzo ya maanasana, Imam Ali AS anatupa somo muhimu la namna ya kuziteka nyoyo na kuvutia marafiki. Kiujumla hapa Imam anazungumzia uhalisia wa mambo kwamba, nyoyo za watu muda wote zina woga na wasiwasi na huwa zinamtilia shaka mtu mgeni ambaye hazijamzoea. Hivyo njia bora kabisa ya kuvutia nyoyo za watu ni kuzionesha mapenzi na ukarimu na mara linapofanyika hilo, utauona moyo wa mtu unalainika na kuvutika kwa mtu huyo. Maumbile ya mwanadamu ni kupenda aone anapendwa na anaheshimiwa. Unapomuonesha mapenzi moyo wake hulainika haraka lakini mtu anapoona hapendwi, huiona dunia ni mzigo mkubwa kwake, hujiona mpweke na hukata tamaa na yuko tayari kufanya kila analoweza ili kuvutia mapenzi ya wengine kwa gharama yoyote ile.
Maumbile ya mwanadamu kiasili ni maumbile safi kama yalivyoumbwa na Mwenyezi Mungu. Hayo ya moyo safi ndiyo maumbile ya dhati ya kila mwanadamu na muda wote kiumbe huyu huwa ana kiu ya kupendwa na kupenda. Tab'an kupenda na kupendwa si kazi rahisi kwa watu wengi, hasa wale ambao hawajui maana ya mapenzi. Watu wa namna hiyo hujihisi muda wote kuwa wametengwa lakini wanapoendewa kwa moyo safi, hata na wao nao nyoyo zao hulainika. Mfano wa wazi unaonekana wakati mtu anapohamia katika mji au kitongoji kipya. Mtu huyo huanza kwa kujiweka mbali na majirani zake, lakini kama majirani hao watamkaribisha vizuri na kumuonesha mapenzi, huhisi wamempa zawadi kubwa na moyo wake hufunguka.
Katika dhati yake, mwanadamu ni mtu wa kuishi kijamii na hawezi kabisa kuishi peke yake. Maendeleo yote ya mwanadamu yanaonekana chini ya kivuli cha jamii yake. Tab'an hii haina maana kwamba amuoneshe mapenzi mtu yoyote tu bila ya kumjua undani wake. Baadhi ya wakati mtu anaweza kuwa ni adui yako aliyekusudia kukudhuru, hivyo kuchukua tahadhari ni jambo la wajibu. Suala la mapenzi nalo linahitaji kuandaliwa mazingira yake ni hivyo hivyo uadui nao una maandalizi yake. Kila siku na kila mmoja wetu huwa tunapata fursa nyingi za kuonesha na kuoneshwa mapenzi na waliotuzunguka hasa watu wetu wa karibu. Njia bora kabisa ya kuonesha mapenzi ni kutekeleza nasaha za Bwana Mtume Muhammad SAW aliyetufundisha kwamba, tunapokutana na ndugu yetu Muislamu tumpokee kwa bashasha, tumuweke mahala pazuri na tumwite kwa jina analolipenda kabisa.
Tusisahau kwamba unapompenda mwenzako kwa dhati, mapenzi yako hayo humuathiri sana hata katika mapenzi yake kwa watu wengine, na watu hao wengine nao huathiriwa na mapenzi hayo na kuwaonesha wengine mapenzi makubwa, tahamaki jamii nzima inaishi kwa kupendana.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.