Jul 08, 2024 04:34 UTC
  • Jumatatu, 08 Julai, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe Pili Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria, mwafaka na tarehe 8 Julai 2024.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria, Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia na masahaba zake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo.

Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya.

Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kuingia katika mji wa Kufa na kuzingirwa katika jangwa na Karbala. 

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita aliaga dunia Pierre Paul Broca, msomi wa Kifaransa na mwanzilishi wa elimu ya kraniolojia (elimu ya fuu la kichwa).

Broca alizaliwa Juni 28 mwaka 1824 huko Ufaransa na baada ya kukamilisha masomo ya msingi na sekondari alijiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kusoma taaluma ya tiba na kuhitimi vyema katika fani hiyo. Baada ya kuhitimu masomo Broca alijishughulisha na kazi ya upasuaji akiwa daktai mahiri.

Sambamba na kazi yake hiiyo aliendelea na utafiiti na uhakiki. Utafiti wake huo ulimfanya afikie ugunduzi muhimu. 

Pierre Paul Broca

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo njama ya mapinduzi ya Nojeh iliyokuwa ikisimamiwa na Marekani nchini Iran iligunduliwa na kuzimwa.

Njama hiyo ya mapinduzi iliratibiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) likishirikiana na baadhi ya vibaraka wa jeshi la anga la utawala wa Shah kwa shabaha ya kumuua Imam Ruhullah Khomeini, kuangamiza utawala wa Kiislamu hapa nchini na kumrejesha madarakani Shapur Bakhitiyar.

Waratibu wa njama hiyo ya mapinduzi walikusudia kufanya mashambulizi dhidi ya makazi ya Imam Khomeini mjini Tehran na kumuua na kisha kushambulia kituo cha kuongozea ndege cha uwanja wa Mehrabad. Hata hivyo njama hiyo iligunduliwa na kusambaratishwa na waratibu wa njama hiyo walitiwa mbaroni na kuhukumiwa.

Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini.

Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu.

Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo. 

Kim Il-sung

Tarehe 8 Julai miaka miwili iliyopita, waziri mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe aliuawa kwa kupigwa risasi.

Shinzo Abe (安倍 晋三, Abe Shinzō) alizaliwa mnamo Septemba 21, 1954 na aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia cha Liberal cha Japan kutoka 2006 hadi 2007 na kwa mara ya pili kutoka 2012 hadi 2020. Abe ndiye mwanasiasa aliyekalia kiti cha waziri mkuu wa Japan kwa muda mrefu zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Shinzo Abe alijulikana kimataifa kwa sera za kiuchumi za serikali yake, iliyopewa jina la utani la Abenomics.

Abe aliuawa Julai 8, 2022 karibu 11:30 asubuhi wakati alipokuwa akihutubia kampeni za uchaguzi huko Nara. Abe ni waziri mkuu wa sita wa Japani kuuawa.

Shinzo Abe

 

Tags