Jul 20, 2024 02:16 UTC
  • Jumamosi, 20 Julai, 2024

Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na tarehe 20 Julai 2024 Miladia.

Miaka 214 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi. ***

 

Siku kama ya leo miaka 183 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, moja ya miji maarufu ya Iran, Sayyid Sadruddin Musawi Amili, msomi na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Sayyid Sadruddin Musawi Amili alizaliwa katika moja ya viunga vya mji wa Jabal Amel, nchini Lebanon. Akiwa kijana mdogo alisafiri nchini Iraq ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika hawza ya elimu ya mjini Najaf, alianza kufanya utafiti katika elimu kadhaa kama vile fiqhi, usulul fiqhi na Hadithi na kufikia daraja la juu katika uwanja huo. Sayyid Sadruddin Musawi Amili ameandika vitabu mbalimbali katika uga wa elimu ya sheria, nahawu na mifano ya aya za Qur’an Tukufu. ***

Sayyid Sadruddin Musawi Amili,

 

Katika siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati. ***

Georg Friedrich Bernhard Riemann

 

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Abul Qasim Lahori. Abul Qasim Bin Hussein Bin Naqi Ridhawi Taqawi Lahori na aliyekuwa faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu alizaliwa Kashmir. Alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa nchini India na ameandika vitabu vingi.  Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na 'Burhanu Shaqqul-Qamar wa Raddun-Nayril-Akbar' 'As-Siratul-Mustaqim.' ***

 

Miaka 87 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana  mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya. ***

Guglielmo Marconi

 

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda. ***

Neil Armstrong

 

Na miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo. ***

Erdogan akiwa Cyaprus ya kaskazini

 

Tags