Aug 12, 2024 08:32 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (60)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 60 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 60 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 53.

السَّخَاءُ مَا کَانَ ابْتِدَاءً؛ [فَإِذَا] فَأَمَّا مَا کَانَ عَنْ مَسْأَلَةٍ، فَحَیَاءٌ وَ تَذَمُّمٌ

Ukarimu ni ule unaofanywa bila ya kuombwa, linalofanywa kwa kuombwa si ukarimu tena bali ni muhali au kuogopa lawama. 

Neno al sakhaa limefasiriwa kwa maana ya ukarimu yaani sifa ya ndani ya mwanadamu inayomfanya aweze kutoa mali na kuwapa maskini na watu wanaostahiki bila ya kutarajia chochote kutoka kwao na bila ya kusubiri kuombwa.

Sasa kwa mujibu wa hikma hii yenye maana pana, Imam Ali AS anatufundisha kuwa, utoaji na msaada wa aina yoyote ile unaotolewa baada ya mtu kuombwa huwa si ukarimu tena bali huwa ni kufanya muhali au mtu kuogopa kulaumiwa na wengine kwa kushindwa kuwasaidia wahitaji. Hivyo ukarimu wa kweli ni wa yule mtu ambaye baada ya kujua shida za watu wengine, akajitolea mwenyewe na kwa siri kuwasaidia watu hao kutatua matatizo yao na ikawa hatarajii malipo kutoka kwao wala shukrani zao. Huyu ndiye mtu mkarimu na muungwana wa kweli.

Hikma hii ya 53 ya Imam Ali AS inafanana na ile hadithi ya Bwana Mtume Muhammad SAW aliposema, ukarimu ni akhlaki ya Allah iliyo kubwa.

Vilevile aya ya 273 ya sura ya pili ya al Baqarah inatuonesha watu wanaostahiki kusaidiwa na kuoneshwa ukarimu wa waungwana na waja wema kwa kusema:  Na wapewe mafakiri waliozuilika katika njia za Mwenyezi Mungu, wasioweza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiyewajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayotoa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.

Katika sehemu nyingine ya kuonesha umuhimu wa ukarimu usiotanguliwa na ombi na usiotarajia malipo ni ile hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Sadiq AS ambaye amesema, kundi moja la watu wa Yemen walikwenda kwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Mmoja wa watu hao alizungumza kwa jeuri na kiburi na kutochunga heshima kiasi kwamba pamoja na kuwa Bwana Mtume ni mpole mno, lakini alikasirishwa na tabia ya mtu huyo na kusawijika usoni na kuangalia chini. Hapo hapo Malaika Jibril AS alishuka na kumwambia Mtume, Mola wako amekufikishia salamu na anakwambia, mtu huyu ni mkarimu na daima analisha maskini na wenye haja. Kusikia vile Bwana Mtume SAW hapo hapo alirejea kwenye hali yake ya kawaida, akanyanyua kichwa chake na kusema, lau kama Jibril asingelishuka na kunipa salamu kutoka kwa Allah kwamba wewe ni mkarimu na daima unalisha maskini, basi ningelijiepusha kabisa kukuangalia. Baada ya kusikia hivyo yule mtu alisilimu hapo hapo na akawa miongoni mwa wanaompwekesha Allah.

Tags