Aug 12, 2024 08:35 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (62)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 62 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 62 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 55.

الصَّبْرُ صَبْرَانِ، صَبْرٌ عَلَى مَا تَکْرَهُ، وَ صَبْرٌ عَمَّا تُحِبُّ

Subira ziko za aina mbili, subira kwa unachokichukia na subira kwa unachokipenda.

Katika hikma hii ya 55 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anagusia pande mbili muhimu sana za subira kwa kusema: Subira ziko za aina mbili, kusubiri mbele ya kufanya jambo zuri lakini lenye dhiki kulitenda na subira katika kuacha jambo baya ambalo nafsi yako inalipenda. Yaani:

 الصَّبْرُ صَبْرَانِ: صَبْرٌ عَلَى مَا تَکْرَهُ، وَصَبْرٌ عَمَّا تُحِبُّ.

Kwa hakika aina ya kwanza ya subira inayoashiriwa hapa na Imam Ali AS ni kusubiri mbele ya mashaka na tabu za kufanya ibada na aina ya pili ya subira ni kuvumilia uzito wa kuacha maasi na vile vitu ambayo kawaida nafsi ya mwanadamu inavipenda sana. Hatuwezi kusema aina ipi ya subira kati ya hizo mbili ni nzito zaidi ikilinganishwa na aina ya pili au ipi ni nyepesi zaidi ikilinganishwa na nyingine. Kila kitu kinategemea aina ya ibada na uzito wake na aina ya maasi na ukubwa wa vishawishi vyake. Lakini lisilo na shaka ni kwamba subira inatakiwa katika pande zote mbili upande wa kufanya ibada na upande wa kuacha kufanya madhambi.

 

Tunapozingatia yote hayo tutaona kuwa, kufuata njia ya haki na kuwa imara kwenye njia hiyo hadi kufikia daraja ya juu ya kuwa karibu na Allah, bali hata kwa ajili ya kufikia kwenye nafasi nzuri katika maisha ya duniani, kote huko kunahitajika subira kubwa. Safari ya kufikia huko si nyepesi hata kidogo. Lazima mtu avuke milima na mabonde, misitu na nyika na kupambana na wanyama wakali na hata maharamia ndio aweze kufika huko. Sasa kama mtu atakuwa na subira ndogo, hawezi kudumu kwenye njia hiyo. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana subira na istiqama inahesabiwa na Qur’ani Tukufu kuwa ndiyo njia bora ya kufanikiwa mwanadamu duniani na Akhera. Aya ya 30 ya sura ya 41 ya Fussilat inasema:

«(إِنَّ الَّذینَ قَالُوا رَبُّنَا اللّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَیْهِمُ الْمَلائِکَةُ أَلاّ تَخافُوا وَلا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتی کُنْتُمْ تُوعَدُونَ)

Hakika wale waliosema: Mola wetu Mlezi ni Allah! Kisha wakawa na isitiqama, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

Naam sharti la kwanza kabisa la kushuka msaada wa Malaika kwa watu waumini ni subira na istiqama. Na ndio maana pia katika sura ya 13 ya al Ra’d Mwenyezi Mungu anasema: Na Malaika wataingia kuwasalimia watu wa peponi katika kila mlango. (Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags