Aug 12, 2024 08:37 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha 64 (57)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 64 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Ingawa hii ni sehemu ya 64 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 57.

الْقَنَاعَةُ مَالٌ لَا یَنْفَدُ

Kukinai ni mali isiyo na mwisho.

Katika hikma hii ya 57, Imam Ali AS anazungumzia maudhui nyingine muhimu sana ambayo muda wote imekuwa inahimizwa na Qur’ani Tukufu na Bwana Mtume Muhammad SAW kiasi kwamba imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Ridha AS akisema, maneno ya kwenye hikma hii ya 57 ya Nahjul Balagha yamepokewa kama yalivyo kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Hadithi hiyo imenukuliwa pia na Mutaqqi al Hindi katika kitabu cha Kanzul ‘Ummal.

Kabla ya jambo lolote ni vyema tutoe ufafanuzi wa mistari michache kuhusu neno kukinai. Kukinai ni hali anayokuwa nayo mtu ambayo inamfanya atosheke na vitu vichache katika maisha yake na asiwe na pupa na tamaa ya kutumia zaidi ya vile vitu vya dharura kuendeshea maisha yake yaani kutumia vitu vya anasa na vya ziada ambavyo muda wote huishughulisha akili ya mwanadamu na mwisho kumtumbukiza kwenye mambo ya haramu.

Hiyo ni maana jumla na kwa ya muhtasari ya neno kukinai. Sasa mtu anapokuwa na sifa ya kukinai, ni wazi kwamba anakuwa na utajiri mkubwa na usioisha kabisa kuliko utajiri mwingine wowote duniani, maana huwa halazimiki kunyoosha mkono wa kuwaomba wengine na kujishushia hadhi yake mbele ya viumbe wengine kwa sababu anahitaji kitu kidogo sana kuendeshea maisha yake.

 

Katika hikma ya 44 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anasema, طُوبَى لِمَنْ ذَکَرَ الْمَعَادَ وَعَمِلَ لِلْحِسَابِ وَقَنِعَ بِالْکَفَافِ Hongera kwa mtu ambaye muda wote anakumbuka siku ya kufufuliwa, akaelekeza juhudi zake zote kwa ajili ya kujiandaa na Siku ya Hisabu na akatosheka na kitu kidogo alichoruzukiwa na Muumba wake.

Imepokewa hadhithi nyingine kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW ambapo anasema: Kinaika na anachokuruzuku Allah, utakuwa tajiri mkubwa kuliko watu wote.

Kwenye kitabu cha hadithi cha Biharul Anwar, imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Ali AS akisema: Nimesaka utajiri katika kila kona na sikuupata ila kwenye kukinai.

Amma jambo jingine muhmu ambalo ni muhimu kuligusia hapa ni kwamba, malalamiko na manung’uniko mengi na yasiyoisha kati ya watu wengi duniani, hayatokani na kwamba watu hao wana mali chache au ni maskini katika vitu vya kimaada na kidunia, bali ni kutokana na umaskini wa kutotosheka na kukosa kukinai watu hao. Mtu anaweza kuwa na utajiri wa dunia nzima lakini akawa maskini kuliko watu wote kutokana na kutokinaika na alichoruzukiwa na Muumba. Kesi nyingi za jinai, uvamizi, dhulma na wizi wa mali za watu zinatokana na wahalifu hao kutotosheka na walicho nacho jambo ambalo ni haraka mno kumuingiza mtu kwenye mambo ya haramu.

Ni vyema tumalizie kwa kunukuu kisa kimoja ambacho kinasema, mtu mmoja wa karibu na mfalme alipita njiani na kumuona mtu maskini anakula mboga za jangwani. Yule mtu wa mfalme alimkejeli kwa kumwambia, ungekuwa uko karibu na mfalme usingelilazimika kula majani haya ya jangwani. Yule maskini alimjibu kwa kumwambia na lau kama na wewe ungetosheka na mboga hizi za jangwani, usingelazimika kujidhalilisha na kuwa mtumwa wa mfalme.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags