Aug 20, 2024 02:15 UTC
  • Jumanne, Agosti 20, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 15 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria, mwafaka na tarehe 20 Agosti 2024.

Leo tarehe 30 Mordad kwa kalenda ya Kiirani ni siku ya kumbukumbu ya Allamah Muhammad Baqir Majlisi, alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu.

Allama Majlisi ndiye mwandishi wa kitabu muhimu na mashuhuri cha Bihar al-Anwar. Alionyesha kipaji kikubwa katika masuala ya elimu tangu akiwa mdogo wakati huo akiwa chini ya malenzi na mafundisho ya baba yake. Baba yake alikuwa mwanazuoni, msomi na mchamungu. Histroria inaonyesha kuwa, kipaji cha Allamah Majlisi kilichanua akiwa angali kijana na barobaro. Alipofikisha umri wa miaka 14 alipata idhini  kutoka kwa Mulla Sadra, mwanafalsafa mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu ya kupokea na kunakili Hadithi.

Alllamah Majlisi alikuwa mmoja wa maulamaa wa Kiislamu waliokuwa na taathira chanya na muhimu katika harakati za kisiasa na kijamii katika kipindi cha utawala wa ukoo wa Safavi. Nafasi na daraja ya kielimu aliyokuwa nayo Allamah Majlisi mbele ya matabaka mbalimbali ya watu ilimfanya mtawala Shah Suleiman Safavi ampatie cheo cha Sheikh al-Islam. 

Allamah Majlisi ameandika vitabu vingi, lakini kitabu chake mashuhuri zaidi ni Bihar al-Anwar. Kitabu hiki ni Dairatul Maarif yaani Ensaiklopidia kubwa ya Hadithi ambayo imekusanya masuala yote ya kidini, kihistoria, fikihi, itikadi, tafsiri ya Qur'ani na kadhalika. Kitabu hiki kina zaidi ya hadithi 85,000 zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Ahlul-Baiti wake watoharifu (as).

Ilimchukua Allamah Majlisi miaka zaidi ya 30 kuandika kitabu hiki. Kundi la wanafunzi wa Allamah Majlisi wakiwa chini ya usimamizi wake walikuwa na nafasi muhimu kkatika kuandika na kupatikana kitabu hiki.   

Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels ulidhibitiwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani.

Huu ulikuwa mji mkuu wa kwanza kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani wakati wa kujiriٰ Vita vya Kwanza vya Dunia.

Miaka 32 iliyopita, Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani, ilijitangazia uhuru.

Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.