Jumatano, Agosti 21, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 16 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria, mwafaka na tarehe 21 Agosti 2024 Milaadi.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad.
Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara Uturuki. Pamoja na kuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo.
The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hiyo katika mkataba huo mwaka 1979.
Tarehe 21 Agosti mwaka 1965 yaani katika siku kama hii ya leo miaka 59 iliyopita Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Alabama walifanya maandamano wakitaka kutekelezwa sheria ya haki ya kupiga kura.
Maandamano hayo yalizidisha harakati ya vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi. Harakati hiyo ilianza mwaka 1955 kwa lengo la kupigania usawa kati ya Wamarekani weusi na wazungu na ilimalizika mwaka 1968 baada ya kupasishwa sheria ya haki za kiraia.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969, Masjidul Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni.
Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibika vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili.
Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).
Miaka 33 iliyopita katika siku kama hii ya leo Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru.
Latvia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Latvia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.
Tarehe 21 Agosti inatambuliwa kama Siku ya Kimataifa ya Msikiti.
Upasishwaji wa siku hii ulijiri mwaka 1382 Hijiria Shamsia, sawa na tarehe 22 Agosti mwaka 2003 katika mkutano uliofanyika mjini Tehran na kwa pendekezo la Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la Iran na kupitishwa na Wizara za Mashauri ya Kigeni za nchi za Kiislamu.
Kikao hicho kilifanyika kwa mnasaba wa wiki ya kumbukumbu ya kuchomwa moto Msikiti wa Al-Aqsa na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 21 Agosti mwaka 1969. Katika kikao hicho, nchi za Kiislamu zilitakiwa kutoa himaya kwa misikiti kama mahala patakatifu na kuenzi maeneo hayo.