Jumatano, tarehe 18 Septemba, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 14 Rabiul Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe 18 Septemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita Yazid bin Muawiya aliangamia.
Yazid alikuwa mtawala dhalimu na fasiki na alitawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa.
Katika kipindi cha utawala wake Yazid mwana wa Muawiya alifanya kila aina ya jinai na alitambulikana kwa ufuska. Miongoni mwa jinai zake ni kumuua shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW yaani Imam Hussein bin Ali (AS) na masahaba zake katika ardhi ya Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria, kushambulia kinyama miji mitakatifu ya Makka na Madina na kubomoa nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba.
Katika siku kama ya leo miaka 315 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza.
Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.
Katika siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru.
Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hussein Tabatabai Qomi, fakihi na marjaa mahiri wa Kishia.
Alizaliwa mwaka 1282 Hijria katika mji mtakatifu wa Qom ulioko yapata kilomita 125 kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran. Alisoma masomo yake ya utangulizi na ya msingi ya dini katika mji huo. Baadaye Sayyid Tabatabai alielekea Tehran na kunufaika na drsa na masomo ya Maulamaa wa mji huo. Akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alifunga safari na kwenda katika Hawza ya Najaf nchini Iraq.
Mwanazuoni huyu hakuwa nyuma pia katika uandindishi wa vitabu na baadhi ya vitabu vyake ni Manasik Haj, Dhakhirat al-Ibad na Tariq al-Najat.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba 1947, Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilianzishwa.
CIA ni miongoni mwa mashirika ya kijasusi ya kutisha sana duniani, na lina jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa kuhusu serikali za nchi za kigeni, makampuni na watu binafsi na kuripoti taarifa hizo kwa serikali ya Marekani.
Shirika hili lilichukua nafasi ya Idara ya Huduma za Kimkakati, ambayo iliundwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kuratibu shughuli za kijasusi kati ya matawi mbalimbali ya jeshi la Merekani.
Shirika la CIA, lenye idara na taasisi nyingi na pana, kama wakala wa ujasusi wa serikali ya Marekani, huwasaidia viongozi wa nchi hiyo katika kuingilia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi ya nchi zingine.
Hadi sasa shirika hilo limehusika na mapinduzi ya serikali katika nchi mbalimbali zinazojitawala. Miongoni mwa mapinduzi hayo ni yale ya tarehe 28 Mordad 1332 Hijria Shamsia (19 Agosti 1953) nchini Iran kwa kushirikiana na shirika la ujasusi la Uingereza MI6.
Baada ya tukio la Septemba 11, 2001 lililoharibu majengo pacha (Twin Towers) huko New York, CIA ilipewa jukumu rasmi na la wazi la kuwateka nyara au kuwaua wapinzani wa Marekani duniani kote.