Jan 02, 2025 02:38 UTC
  • Akhamisi tarehe Pili Januari 2025

Alkhamisi tarehe Mosi Rajab 1446 Hijria sawa na tarehe Pili Januari 2025.

Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele.

Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.”

Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu.

Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab. 

Siku kama ya leo miaka 1389 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake.

Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu.

Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. 

Siku kama hii ya leo miaka 180 posta ya kwanza yenye muundo wa kisasa ilifunguliwa huko Vienna mji mkuu wa Austria.

Kabla ya kuanzishwa chombo makhsusi kwa ajili ya kusafirisha barua na vifurushi vya posta, mizigo hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwa kutumia farasi, ngamia au boti makhsusi. Hata hivyo miaka mingi baadaye kulibuniwa mbinu mpya na mfumo wa posta ukaboreshwa zaidi na kuwa na sura ya sasa.   ****

Katika siku kama ya leo miaka 159 iliyopita leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia.

Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford.

Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'. 

Gilbert Murray

Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia.

Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana.

Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii.   

Isaac Asimov

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 2 Januari 1971, washabiki wa soka wasiopungua 66 nchini Scotland walifariki dunia baada ya kuanguka uzio wa uwanja wa Ibrox Park mjini Glasgow.

Watu wengine zaidi ya 200 walijeruhiwa. Maafa hayo yalitokea wakati wa kuchezwa mechi kati ya mahasimu wawili wakuu wa soka nchini humo, klabu ya Celtic na Rangers.    ****

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi.

Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu."

Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu." 

Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita yaani tarehe Pili Januari 2016 utawala wa Saudi Arabia ulimuua mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al-Nimr. 

Baqir al Nimr aliyekuwa mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia alizaliwa tarehe 21 Juni mwaka 1959 katika mji wa Awwamiyya huko mashariki mwa Saudi Arabia. Alipata elimu ya msingi katika mji huo na mwaka 1400 Hijria yaani mwaka 1989 alielekea Tehran nchini Iran na kupata elimu katika chuo cha kidini cha Qaim kilichoasisiwa na Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi. Baada ya kupata elimu katika chuo hicho kwa kipindi cha miaka 10 Sheikh Nimr alikwenda Syria na kuendelea kutafuta elimu zaidi katika Chuo cha Kidini cha Bibi Zainab (as).

Aliporejea Saudi Arabia, Sheikh Nimr aliasisi kituo cha kidini cha al Imam al Qaim katika mji wa Awwamiyya ambacho kiliweka jiwe la msingi la kuanzishwa Kitiuo cha Kiislamu hapo mwaka 2011.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu daima alikuwa akikosoa siasa za ukandamizaji na kibaguzi za utawala wa kifalme wa Saudia na alifungwa jela mara kadhaa kutokana na kusema haki na kweli.

Mara ya mwisho Sheikh Baqir Nimr alikamatwa tarehe 8 Julai mwaka 2012 katika maandamano makubwa ya Waislamu wa Kishia ya kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud na tarehe 15 Oktoba msomi huyo wa Kiislamu alihukumiwa kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo.

Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016. Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu. 

Sheikh Baqir Nimr

Na miaka 5 iliopita katika siku kama ya leo, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliuawa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq kwa amri ya moja kwa moja ya Rais Donald Trump wa Marekani.

Shahidi Qassim Suleimani alizaliwa tarehe 20 Isfand 1335 Hijria Shamsia katika mji wa Kerman.  Wakati wa utoto na kuinukia kwake aliupitisha akiwa pamoja na baba yake. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH alijiunga na kikosi hicho.

Wakati wa kuanza vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Qassim Suleimani akawa akitoa mafunzo kwa brigedi za kijeshi mjini Kerman na kuzituma katika medani ya vita. Mwaka 1360 Qassim Suleimani akateuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharallah. Kikosi hicho chini ya uongozi w Qassim Suleimani kilitekeleza operesheni nyingi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu kama Walfajr 8, Karbala 4, Karbala 5 na kadhalika. Mwaka 1389 akateuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa, Kamnada wa Kikosi cha Qusd cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.

Baada ya kuibuka kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria, Luteni Jenerali Qassim Suleimani alihudhuria katika medani za vita za mataifa hayo akiitikia wito wa viongozi wa nchi hizo na kuwa na nafasi kubwa katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi.

Hatimaye aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020 pamoja na Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao wengine wanane katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump.

Luteni Jenerali Shahidi Qassim Suleimani