Jan 11, 2025 02:55 UTC
  • Jumamosi, 11 Januari, 2025

Leo ni Jumamosi 10 Rajab 1446 Hijrai ambayo inasadiifiana na 11 Januari 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua. Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar.  

 

Tarehe 10 Rajab miaka 1251 iliyopita,  alizaliwa Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Taqi Al-Jawad (as) alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha (as). Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui."

 

Siku kama ya leo miaka 700 iliyopita mji wa Mexico ambao hivi sasa ni mji mkuu wa nchi ya Mexico, uliasisiwa na mmoja wa wafalme wa silsila ya Aztec. Waaztec walikuwa miongoni mwa makabila ya Wahindi Wekundu wa Amerika ya Latini ambao waliwasili huko Mexico katika karne ya 12 na kutawala eneo hilo mwanzoni mwa karne hiyo.

 

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, sawa na tarehe 22 Dei 1313 Hijiria Shamsia, alifariki duania akiwa na umri wa miaka 79 Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani mmoja wa maulama wakubwa. Awali alianza kusoma mjini Isfahani kwa wasomi wakubwa kama vile Ayatullah Mirza Abul-Maali Kalbasi na Ayatullah Muhammad Baqer Masjid Shahi na baadaye akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukukamilisha masomo yake ya Kiislamu. Baadaye Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani alirejea mjini Isfahan na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji, uandishi na kufanya tablighi ambapo maulama wakubwa zaidi ya 300 walikuwa wakisoma kwake. Mbali na uga wa elimu, msomi huyo alikuwa hodari katika kutoa hotuba ambapo alikuwa akiwalingania watu wa matabaka tofauti. Miongoni mwa athari za Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani ni kitabu cha 'Sharhu Sharaai' chenye juzuu mbili, 'Jannatul-Maw'a' kinachohusu Akhlaaq, 'ufafanuzi wa tafsiri ya Swaafi' na 'Wasiilatun-Najaat.' 

Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani

 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu Amrehemu Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliagiza kuundwa Baraza la Mapinduzi katika kipindi hicho muhimu cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Imam aliagiza baraza hilo liundwe wakati Marekani ilipokuwa ikifanya njama za kuulinda utawala wa kifalme wa Pahlavi. Jukumu kubwa la baraza hilo lilikuwa ni kuratibu mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia kuandaa uwanja mzuri wa kuundwa serikali ya muda nchini Iran. Katika ujumbe wake Imam Khomeini alisema: "Takwa la wananchi Waislamu wa Iran si tu ni kuondoka Shah na kuung'oa madarakani mfumo wa kifalme, bali ni kuendeleza mapambano ya taifa la Iran na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu ambayo itaambatana na uhuru wa kitaifa na kujitegemea nchi hii na pia kudhamini uadilifu wa kijamii."

 

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita sawa na tarehe 11 Januari mwaka 1992, Rais Shazli bin Jadid wa Algeria alijiuzulu baada ya Harakati ya Uokovu wa Kiislamu ya Algeria (FIS) kupata mafanikio makubwa katika uga wa kisiasa na matukio ya baadaye nchini humo. Rais Shazli alichaguliwa kuwa rais wa Algeria mwaka 1979 baada ya kifo cha Houari Boumediene, rais wa zamani wa nchi hiyo. Mwaka 1988 Shazli bin Jadid aliahidi kutekeleza marekebisho na kufanya mabadiliko ya katiba ya Algeria, ambapo kwa mujibu wake suala hilo lingetoa mwanya wa kutambuliwa rasmi vyama vya kisiasa. 

Shazli bin Jadid

 

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, mhadhiri wa nyuklia wa Chuo Kikuu cha Tehran, Dokta Massoud Ali-Mohammadi aliuawa kigaidi. Massoud Ali-Mohammadi aliyekuwa na umri wa miaka 50 aliuawa kwa mlipuko wa bomu la kuongozwa kutoka mbali wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake. Alipata shahada ya uzamivu ya taaluma ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Sharif mjini Tehran mwaka 1371 na alikuwa miongoni mwa wanachuo wa kwanza wa Iran kupata shahada ya uzamivu ya somo la fizikia ndani ya Iran. Alitunukiwa tuzo ya Tamasha ya Kimataifa ya Kharazmi mwaka 1386 na kushika nafasi ya pili katika utafiti wa masuala ya kimsingi. Wapinzani wa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya kushindwa kusimamisha miradi hiyo kwa hatua za kisiasa na vikwazo vya kiuchumi walikhitari kutumia njia za kigaidi na kuwaua wasomi wa nyuklia wa Iran. Magaidi waliomuua msomi huyo wa Iran walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walikuwa wakishirikiana na utawala haramu wa Israel.

Massoud Ali-Mohammadi