Jumapili, Pili Februari, 2025
Leo ni Jumapili tarehe Tatu Shaaban 1446 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe Pili Februari 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake Imam Hassan (as). Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) uliwasili katika mji wa Makka. Imam Hussein ambaye alikuwa amehatarisha maisha yake kwa kuupinga utawala wa Yazid na kukataa kumpa baina na mkono wa utiifu kiongozi huyo, aliondoka Madina na kuelekea Makka. Alipowasili mjini Makka Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib alilakiwa na watu wengi na shakhsia wakubwa wa mji huo na akaamua kuitumia fursa ya uwepo wa Mahujaji kwa ajili ya kufichua ufisadi wa Bani Ummayah hususan Yazid bin Muawiya na kwa muktadha huo akawa amefikisha ujumbe wake katika pembe mbalimbali za maeneo ya Waislamu. Aidha akiwa mjini Makka Imam Hussein alipokea maelfu ya barua kutoka kwa wakazi wa mji wa Kufa Iraq ambao mbali na kutangaza kuupinga utawala wa Yazid walimtaka Imam aelekee katika mji huo. Baada ya kukaa kwa takribani miezi mine mjini Makka na kwa kuzingatia mwaliko wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili kutoka kwa makachero wa Yazid, tarehe 8 Dhulhija mwaka 60 Hijria, alielekea katika mji wa Kufa.

Miaka 233 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa kihistoria wa Berlin, ulitiwa saini baina ya Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia. Mkataba huo ulikuwa natija ya maafikiano baina ya viongozi hao wawili yaliyofikiwa tarehe Pili Agosti mwaka 1791 huko Pillnitz kwa ajili ya kukabiliana na mapinduzi ya Ufaransa. Hii ilitokana na kuwa, watawala wa Ulaya walikuwa wameingiwa na woga mkubwa kutokana na baadhi ya nadharia za wapigania uhuru wa Ufaransa. Licha ya kuweko mkataba huo na hata mashambulio ya pamoja ya Austria, Prussia na Uingereza dhidi ya Ufaransa na himaya yao kwa wapigania mfumo wa utawala wa Kifalme wa nchi hiyo, harakati hizo hazikuwa na natija kwani hatimaye wanamapinduzi wa Ufaransa waliibuka na ushindi.

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita alizaliwa Ayatullah Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi na ya kati alielekea Najaf, Iraq na kupata elimu kwa maulama wakubwa wa zama. Alifikia daraja ya ijtihadi akiwa na umri wa miaka 26 na baada ya kurejea Isfahani alijikita katika shughuli ya kufundisha sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake wavue vazi la staha la hijabu, Ayatullah Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, Dmitri Ivanovich Mendeleev msomi na mwanakemia wa Kirusi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Saint Petersburg uliokuwa mji mkuu wa Russia wakati huo. Dmitri alizaliwa mwaka 1834 na kusoma taaluma ya kemia. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mwingi muhimu katika taaluma ya kemia ambapo baadaye ulikuja kujulikana kwa jina la jedwali la Mendeleev.

Tarehe 14 Bahman 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama hii ya leo miaka 46 iliyopita, wananchi wa Iran walipokuwa katika sherehe na shamrashamra za kurejea nchini Imam Khomeini akitokea uhamishoni nje ya nchi, Imam alizungumza na waandishi habari akieleza misimamo ya mfumo ujao wa utawala wa Kiislamu hapa nchini na kutangaza kuwa ataunda serikali ya mpito ya mapinduzi muda mfupi baadaye. Imam Khomeini alitangaza kuwa serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kutayarisha kura ya maoni ya Katiba mpya ya Iran. Vile vile alimtahadharisha Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah kwamba, iwapo ataendelea kuwakandamiza wananchi angetangaza vita vya jihadi. Imam Khomeini vile vile alilitaka jeshi lijiunge na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo pia ilitangazwa kwamba, Wamarekani elfu 35 walikuwa wamekwishaondoka katika ardhi ya Iran na kwamba wengine elfu 10 wako mbioni kuondoka. ***

Katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha kwa mafanikio roketi ya kwanza ya kupeleka satalaiti angani iliyojulikana kwa jina la Omid. Miaka iliyofuata Iran ilituma viumbe hai angani kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kobe na tumbili, na hatua hiyo iliingiza Iran katika klabu ya nchi zenye teknolojia ya anga za mbali tena katika kipindi hicho cha vikwazo vikali vya kiuchumi vya nchi za Magharibi. ***
