Alkhamisi, tarehe 6 Februari, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 07 Shaabani 1446 Hijria, sawa na Februari 6 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 408 iliyopita alifariki dunia daktari na mtaalamu wa mimea wa Italia, Prospero Alpini.
Alizaliwa mwaka 1553 na baada ya kuhitimu masomo ya tiba alitunukiwa shahada ya udaktari. Katika uchunguzi na utafiti wake, Prospero Alpini aligundua kwamba, mimea kama walivyo wanyama, ina jinsia mbili za kike na kiume japokuwa hakuweza kujua kama kanuni hiyo inahusu kila kitu.
Miongoni mwa hatua nyingine muhimu za Prospero Alpini ni kuarifisha kahawa na ndizi kwa watu wa Ulaya. Biashara ya kahawa ya Mocha au al Mukha ambalo ni jina la bandari iliyoko kusini mwa Yemen, ilikuwa mikononi mwa Waislamu tangu karne ya 15, na mtaalamu huyo wa mimea wa Italia ndiye aliwajulisha watu wa Ulaya aina hiyo ya kahawa (Arabica) iliyokuwa ikioteshwa katika maeneo ya milimani nchini Yemen.

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita mkutano wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za sumu ulimaliza kazi zake mjini Washington, Marekani kwa kutiwa saini mkataba uliopewa jina la mkataba wa pande tano kati ya nchi zilizoshiriki mkutano huo.
Nchi zilizotia saini mkataba huo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Japan. Mkataba huo ulipiga marufuku utumiaji wa aina yoyote ya gesi za sumu na za kemikali katika vita. Miaka kadhaa baadaye nchi nyingine zilijiunga na mkataba huo wa kuzuia utumiaji wa gesi za sumu vitani.

Miaka 89 iliyopita mwafaka na tarehe 6 mwezi Februari mwaka 1936 eneo lenye baridi zaidi duniani lilitambuliwa na jopo moja la kielimu baada ya kufanya juhudi za miaka minne na hatimaye kugundua eneo hilo.
Kundi hilo la wataalamu hatimaye liligundua kuwa, mji wa Verkhoyansk huko Siberia, kaskazini mwa Russia, ndiyo eneo lenye baridi zaidi duniani baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu. Mji wa Verkhoyansk ulikuwa ukitumika kama makazi ya uhamishoni ya wahalifu wa kisiasa wa Russia kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti.
Mji huo una jamii ndogo ya watu ambao kazi yao kuu ni biashara ya ngozi na kuchimba madini. Kiwango cha joto la eneo hilo majira ya baridi hufikia daraja 70 chini ya sifuri. ***
Tarehe 6 Februari miaka 62 iliyopita aliaga dunia mwanaharakati mashuhuri na mpigania uhuru wa Morocco, Abd-el Karim Al-Khattabi.
lianzisha harakati za kupambana na wakoloni wa Kihispania na Kifaransa akiwa bado kijana na kuunda kundi la mapambano katika maeneo ya milimani nchini humo.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia Uhispania ilifanya mauaji mengi ya halaiki huko Morocco kwa ajili ya kupanua mamlaka na ushawishi wake.
Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na wakati wa kupamba moto mapambano ya wanamapinduzi wa Morocco, Ufaransa nayo ilifanya mauaji dhidi ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo.

Na tarehe 18 Bahman miaka 41 iliyopita aliuawa Jenerali Gholam-Ali Oveissi aliyehusika na mauaji ya wananchi wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Jenerali Oveissi ambaye alikuwa Kamanda Mkuu wa jeshi la utawala wa kifalme wa Shah alihusishwa na mauaji ya wananchi wa Iran mwaka 1962 na 1978 katika vuguvugu la wananchi wa Iran la kutaka kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu na kuuondoa madarakani utawala wa dhalimu wa kifalme.
Oveissi alikimbia nchi mwezi mmoja kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hata kabla ya Shah Pahlavi kutoroka nchi. Mwezi mmoja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jenerali Oveissi alifanya jitihada za kuwakusanya tena waungaji mkono wa utawala wa kifalme nchini Iran na kutoa dharba kwa Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo njama hizo zilishindwa na hatimaye kibaraka huyo wa Shah aliuawa katika siku kama hii leo akiwa Paris nchini Ufaransa.
