Feb 10, 2025 02:39 UTC
  • Jumatatu, 10 Februari, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Shaaban 1446 Hijria, sawa na tarehe 10 Februari 2025.

Siku kama ya leo miaka 1413 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina.

Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake, Mtume Mtukufu (saw), alinufaika na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake, Imam Ali (as), na baba yake, Imam Hussein (as).

Ali bin Hussein alikuwa maarufu kwa jina la Ali al Akbar yaani Ali Mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma za utawala wa Bani Umayyah.

Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo inatambiliwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Vijana.   

Siku kama ya leo miaka 917 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran.

Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala.

Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kutunga na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika kutunga mashairi.

Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi. Ndani ya kitabu hicho Ghaznawi ameweka wazi fikra zake za kiakhlaqi na irfani. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.   

Siku kama ya leo miaka 262 iliyopita ulitiwa saini mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa katika mji wa Paris. Wafaransa waliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana. Hii ni kutokana na kuwa, baada ya miaka mingi ya vita na mivutano na Uingereza, Ufaransa ilikubali kufumbia macho madai yake yote na maslahi yake ya kikoloni huko India na Canada. 

Sababu ya kutiwa saini mkataba huo ni kwamba, katika kipidi hicho Ufaransa ilikuwa imedhoofika kutokana na kujihusisha na vita mbalimbali barani Ulaya, na kwa upande wa kijeshi na kiuchumi haikuwa na ubavu wa kuendelea kupigana vita na Uingereza. ***

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alifariki dunia Sophia Krukovsky mwanahisabati wa Russia. 

Alizaliwa mwaka 1850 mjini Moscow. Licha ya kuwa alipendelea sana elimu ya hisabati, lakini kutokana na sababu za kibaguzi hakuweza kujiunga na chuo kikuu na ni kwa msingi huo ndio maana akaelekea nchini Ujerumani na kujifunza elimu ya hisabati na fizikia. Pamoja na hayo Sophia Krukovsky alikabiliwa na matatizo mengi kabla ya kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu. Kufuatia hali hiyo alilazimika kusoma elimu hiyo kwa mwalimu wa hisabati nje ya chuo kikuu.

Mwaka 1874 Sophia Krukovsky alitunukiwa shahada ya juu ya Uzamivu (PhD) bila kuhudhuria chuoni. Mwaka 1888 alitunukiwa zawadi yenye itibari katika chuo cha academia nchini Ufaransa. Kuanzia mwaka 1884 hadi mwaka 1891 alipofariki dunia alijishughulisha na kazi ya ufundishaji wa hisabati katika Chuo Kikuu cha Stockholm, Sweden.

Sophia Krukovsky

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, tawala za waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia zilisaini makubaliano ya amani.

Katika siku hiyo, Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa zilisaini makubaliano ya amani na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo yaani Italia, Finland, Poland, Hungary, Romania na Bulgaria, na kwa utaratibu huo nchi sita hizo kwa mara nyingine tena zikajipatia uhuru. ***  

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita yaani tarehe 10 Februari mwaka 1950, Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomunisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani.

Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "Mc Carthisim" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani.

Kamisheni ya Mc Carthisim ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi. 

Joseph Mc Carthy

Tarehe 22 Bahman miaka 46 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote.

Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi.

Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme.

Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote.

Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500.