Jumanne, 4 Machi, mwaka 2025
Leo ni Jumanne tarehe 3 Ramadhani 1446 Hijria sawa na tarehe 4 Machi mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1033 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Muhammad bin Nu'man mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad.
Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh.

Katika siku kama ya leo miaka 879 iliyopita aliaga dunia Ibn Khashhab mhakiki na mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria.
Alizaliwa mwaka 492 Hijria huko Iraq na kuanza kujifunza masomo ya zama hizo tangu akiwa mdogo. Ibn Kashshab hatua kwa hatua alijifunza masomo ya mantiki, hadithi na uandishi na kuanza kuandika vitabu mbalimbali katika nyanja hizo.
Ibn Khashshab alikuwa shakhsiya wa aina yake na ndio maana akafahamika sana kwa jina la Allamah. Aidha alitajwa kama bwana wa maqarii wa zama zake kutokana na umahiri wake katika kusoma na kufahamu vyema Qur'ani Tukufu.

Tarehe 4 Machi miaka 202 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ugiriki vilifanya mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waislamu elfu 12 wakati wa vita vyao dhidi ya jeshi la ufalme wa Othmania katika mji wa Tripolitsa.
Makundi ya Wagiriki waliokuwa wakiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, yaliungana na kutekeleza mauaji hayo katika muongo wa mwanzoni mwa karne ya 19, yaani mwaka 1822. Kufuatia mauaji hayo mwezi Novemba mwaka 1824 majeshi ya utawala wa Kiothmani yaliamua kulipiza kisasi kwa kuua kundi la Wagiriki. ***
Na siku kama ya leo miaka 58 iliyopita sawa na tarehe 14 Esfand mwaka 1346 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Dakta Muhammad Musaddiq, Waziri Mkuu na mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Iran.
Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1261 Hijria Shamsia. Mwaka 1299 Hijria Shamsia ikiwa ni baada ya kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje, Musaddiq alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Tehran bungeni.
Alifanya jitihada kubwa za kutaifishwa sekta ya mafuta nchini Iran na mwaka 1329 Hijria Shamsia alifanikiwa kupasisha kanuni ya kutaifishwa mafuta bungeni kwa himaya ya makundi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Kashani. Baadaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria na kufungwa jela miaka mitatu.
Baada ya kutumikia kifungu hicho Musaddiq alibaidishiwa katika kijiji kimoja huko magharibi mwa Tehran na alifariki dunia miaka kadhaa baadaye katika siku kama ya leo.

Na Tarehe 4 Machi inajulikana kama Siku ya Kupambana na Unene Duniani (World Obesity Day) katika kalenda ya kimataifa.
Siku ya Unene Duniani, ambayo hadi 2020 iliadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka, ilianzishwa kwa ushirikiano wa Shirikisho la Unene Duniani ili kutoa masuluhisho ya vitendo ya kusaidia watu kufikia uzito wa afya, kupata matibabu sahihi na kushughulikia tatizo la unene. Siku hiyo pia huadhimishwa ili kuongeza ufahamu kuhusu magonjwa hatari zaidi yanayohusishwa na unene unaoathiri watu duniani kote.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha unene wa kupindukia kimeongezeka mara tatu tangu 1975 na kimeongezeka mara tano kwa watoto na vijana, na hali hii inaendelea katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
Kwa sasa zaidi ya 35% ya idadi ya watu duniani wana unene wa kupindukia, na kama hali hii itaendelea, 50% ya idadi ya watu duniani itakuwa na unene wa aina hiyo ifikapo 2035.
Siku hii imeainisha ili kukumbusha tatizo hili na kutafuta njia za kurekebisha.
Lishe nzuri, mazoezi, kuweka malengo halisi, na ufuatiliaji wa uzito mara kwa mara ni miongoni mwa njia za kupambana na unene wa kupundukia.
