Jumatatu, 10 Machi, 2025
Leo ni Jumatatu 9 Ramadhani 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 10 Machi 2025.
Siku kama ya leo miaka 593 iliyopita, alifariki dunia Ologh Beig, msomi mkubwa wa elimu ya nyota.
Alizaliwa mwaka 796 Hijiria eneo la Soltaniyeh, moja ya miji ya magharibi mwa Iran na kulelewa katika taasisi ya babu yake, Timur ambayo ni moja ya silsila ya utawala wa Timur.
Akiwa na umri wa miaka 16 aliteuliwa kuwa kamanda wa jeshi katika eneo la Mā warāʼ al-Nahr (Transoxiana), katikati mwa Asia. Kinyume na utawala wa Timur, yeye hakupendelea kupanua dola hilo na badala yake akajikita katika utafiti na utalii. Katika kipindi hicho aliasisi kituo cha kielimu ambacho kilitoa elimu ya nyota.
Aidha hatua yake nyingine ilikuwa ni kujenga kituo cha kufuatilia nyota huko katika mji wa Samarqand hapo mwaka 828 Hijiria, ambacho kilitoa wasomi wengi wa masuala ya nyota.
Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani, Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake, Thomas Watson.
Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano. Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka.
Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo.
Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo.
Hata hivyo Japan haikusalimu amri hadi Mwezi Agosti mwaka huo huo wa 1945 wakati Marekani iliposhambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuua maelfu ya raia wasio na hatia.

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita alifariki dunia Konstantin Ustinovich Chernenko, kiongozi wa zamani wa Urusi ya Zamani.
Alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1911 Miladia katika familia ya kawaida na ya kijijini maeneo ya Siberia ambapo baada ya kuhitimu masomo yake na akiwa na umri wa miaka 18 alijiunga na idara ya vijana ya chama cha Ukomonisti, huku akiwa mwanachama rasmi miaka miwili baadaye.
Kwa kipindi cha miaka 20 alikuwa mjumbe wa ngazi ya juu wa ofisi ya kisiasa wa chama cha Ukomonisti wa Urusi ya zamani na baada ya hapo akateuliwa kuwa katibu Mkuu. Aidha katika kipindi chote cha utawala wa Leonid Ilyich Brezhnev alikuwa akiandamana na Konstantin Ustinovich Chernenko na ni kwa ajili hiyo ndipo Wamagharibi wakamwita Chernenko kuwa ni kivuli cha Brezhnev.
Baadaye alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo na kufanikiwa kuongoza kwa kipindi cha miezi 13 na kufariki dunia katika siku kama ya leo mwaka 1985 akiwa na umri wa miaka 74. Ni baada ya kufariki dunia ndipo akachaguliwa Mikhail Sergeyevich Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Urusi ya zamani.