Mar 12, 2025 02:34 UTC
  • Jumatano, 12 Machi, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 11 Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Machi, 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 593 iliyopita, alifariki dunia mjini Cairo Ibrahim Karaki, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na Hadithi wa Kiislamu.

Baada ya kusoma Qur'ani na masomo ya awali ya kidini, Ibrahim Karaki alianza kufanya safari katika maeneo mbalimbali katika vituo vya elimu ya kidini kwa lengo la kukamilisha masomo yake ya juu kama vile fiqihi na fasihi ya lugha ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo.

Kitabu cha I'rabul-Mafsal ni miongoni mwa athari zilizoachwa na msomi huyo.

Miaka 171 iliyopita katika siku kama hii ya leo mkataba wa kihistoria wa Constantinople (Istanbul) ulitiwa saini baina ya Ufaransa, Uingereza na utawala wa kifalme wa Othmaniyyah.

Baada ya nchi hizo tatu kutia saini mkataba huo dhidi ya sera za kujitanua za Urusi ya zamani huko Ulaya, zilipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata ushindi dhidi ya Urusi katika vita vya Crimea. 

Miaka 100 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Sun Yat-sen mwanamapinduzi na Rais wa Kwanza wa China.

Sun Yat-sen anayejulikana kama baba wa taifa la China alizaliwa mwaka 1866 huko Nanlang China. Mwaka 1892 alijiunga na Chuo Kikuu na akiwa na umri wa miaka 26 alifanikiwa kupata shahada ya udaktari. Uwanja na mazingira ya Sun Yat-sen ya kuanzisha harakati zake za kisiasa yaliandaliwa baada ya Japan kuishambulia China mnamo mwaka 1894. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanzisha harakati zake dhidi ya mfumo wa kifalme wa Manchu. Baada ya harakati hiyo kushindwa alikimbilia nje ya nchi.

Mwaka 1905 alirejea China na kuanzisha Muungano wa Wanamapinduzi wa China lengo likiwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1911 utawala wa familia ya kifalme ya Manchu ulifikia tamati baada ya kupinduliwa. Tukio hilo lilipelekea kutangazwa mfumo wa Jamhuri nchini China na Sun Yat-sen alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China. 

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India.

Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini.

Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali.

Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake. 

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao.

Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja.