Alkhamisi, Machi 20, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Machi mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita mwaka 40 Hijria Qamaria, Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume muhammad SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiwa katika Swala ya Alfajiri katika Msikiti wa mji wa Kufa nchini Iraq na mtu aliyeitwa Abdur Rahman bin Muljim al Muradi.
Imam Ali A.S alikufa shahidi siku 3 baada ya tukio hilo.
Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa shujaa, aliyekuwa na imani halisi, akhlaki njema, elimu na uadilifu wa kupigiwa mfano. Alipata elimu na malezi kwa Mtume Muhammad mwenyewe SAW, na alikuwa mwanamume wa kwanza baada ya Mtume SAW kuukubali Uislamu.
Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na alihatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume na dini ya Uislamu. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo mkubwa.
Imam Ali AS alipenda haki na uadilifu na kupambana vilivyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima Amirul Muuminin AS anasema: 'Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake Siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wa Mungu.'

Tarehe 20 Machi miaka 298 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84.
Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.

Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 20 Machi 1956, nchi ya Tunisia iliyoko katika eneo la kaskazini mwa Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa.
Ijapokuwa harakati za ukombozi nchini humo zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini kutokea Vita vya Pili vya Dunia na kudhoofika Ufaransa kwenye vita hivyo, kuliandaa mazingira mazuri ya kujikomboa nchi hiyo. Baada ya kujipatia uhuru, Habib Bourguiba aliongoza nchi hiyo, kwa karibu miongo mitatu lakini kwa mabavu na ukandamizaji.
Baada ya utawala wa Bourguiba, nchi hiyo ilitawaliwa na Zainul Abidin Ben Ali ambaye aliingia madarakani mwaka 1982. Kiongozi huyo naye alifuata mbinu na mwendo uleule wa Bourguiba wa kuwakandamiza wananchi na kupiga vita Uislamu, suala lililopelekea wananchi wa nchi hiyo kusimama kidete na kumng'oa madarakani mwezi Januari mwaka 2011.

Na siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, vikosi majeshi ya waitifaki wa Marekani na Uingereza viliishambulia Iraq kwa kisingizio kwamba nchi hiyo inazalisha silaha za mauaji ya umati.
Hatua hiyo ilichukuliwa licha ya malalamiko makubwa ya walimwengu. Kufuatia vita hivyo vya umwagaji damu, zaidi ya makombora 1000 ya cruise, maelfu ya mabomu na makumi ya maelfu ya mizinga na mabomu ya vishada yalimiminiwa wananchi wasio na hatia wa Iraq. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wa Kiiraqi waliuawa katika vita hivyo.
Aidha nyumba zisizo na idadi za Wairaqi, hospitali, taasisi za kiuchumi, kiutamaduni na misikiti ilibomolewa.
