Apr 03, 2025 02:29 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 3 Aprili, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 03 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani, alivuliwa madaraka na Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani.

Licha ya kuondolewa madarakani, aliendelea kubaki kwenye wadhifa huo kwa muda mchache, lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia mwaka 1898.

Otto Von Bismarck

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Aprili 1941, mji wa Baghdad ulikombolewa na Rashid A'li Gilani kiongozi wa mrengo uliokuwa ukiwapinga Waingereza, baada ya kujiri mapigano kati ya wazalendo wenye uchungu wa nchi yao dhidi ya serikali ya London.

Gilani alikuwa akiungwa mkono na Ujerumani na kutokana na kutopata misaada kwa wakati mwafaka, vikosi vya Uingereza vilifanikiwa kuwakandamiza wafuasi wa wake.

Baada ya tukio hilo serikali ya Iraq ilijiunga na nchi waitifaki katika Vita vya Pili ya Dunia.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Zakir Hussein Rais Mwislamu wa India aliaga dunia.

Zakir Husain alizaliwa 1897. Alisoma masomo yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh na baadaye alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Berlin nchini Ujerumani. Kwa miaka mingi alijihusisha na harakati za kielimu na kisiasa.

Mwaka 1962 aliwa Makamu wa Rais wa India. Hatimaye mwaka 1967 alichaguliwa kuwa Rais kupitia uchaguzi wa wananchi. Zakir Husain alikuwa mpinzani mkubwa wa vitendo vya mabavu vya Wahindu dhidi ya Waislamu na alikuwa miongoni mwa shakhsia walioafiki suala la Pakistan kujitenga na India. 

Zakir Husain

Siku kama ya leo miaka 23, iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina.

Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina.

Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.