Jun 09, 2025 02:11 UTC
  • Jumatatu, Juni 9, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria sawa na Juni 9 mwaka 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1957 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Juni mwaka wa 68 Miladia, Mfalme Nero Claudius Caesar mtawala katili na aliyemwaga damu nyingi wa Rome alijiua, baada ya kuishi kwa miaka 31 na kutawala kwa maiaka 14.

Si vibaya kuashiria hapa kwamba Nero aliasiliwa na mjomba wake Mfalme Claudius aliyekuwa mtawala wa kwanza wa Rome. Lakini Nero alimpa sumu mfalme huyo na kuchukua nafasi yake baada ya kufa.

Mfalme huyo katili na wa mwisho wa Rome, wakati wa utawala wake aliwaua watu wengi wa familia yake akiwemo mama yake, mkewe, kaka yake na ndugu zake wengine. Pia aliwaua wananchi wake wengi. Aliwaua kwa umati Wakiristo pamoja na kuuchoma moto mji wa Rome. 

Nero

Miaka 140 iliyopita muwafaka na leo, jeshi la Ujerumani lilivamia ardhi ya Togo huko magharibi mwa Afrika.

Wakati huo maeneo ya pwani ya Togo yalipendelewa zaidi na watu wa Ulaya kwa ajili ya biashara ya utumwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Togo imekuwa maarufu kwa jina la "Pwani ya Utumwa."

Wakoloni wa Ujerumani waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Togo hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya hapo Togo ilikoloniwa na Wafaransa na Waingereza. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1960. 

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria.

Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra.

Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria.

Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto kadhaa iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisababishwa na jeshi la siri la Ufaransa.   ***

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Elahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani.

Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa Tabrizi huko kaskazini mwa Iran mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea  Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa, Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kupata elimu ya dini katika mji huo.

Baada ya kutabahari katika taaluma za Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na malezi na kueneza elimu na maarifa yya Kiislamu. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Uhusiano wa Kimaanawi Baina ya Roho na Sauti.   

Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Elahi Tabatabai

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu.

Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8.   

Allamah Agha Bozorge Tehrani, (katikati)