Ijumaa tarehe Mosi Agosti 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 7 Safar 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Agosti 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 1397 iliyopita, yaani tarehe 7 Safar mwaka 50 Hijiria kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).
Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake, Mtume Muhammad (saw) ambapo alinufaika na mafunzo na maarifa ya dini tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as).
Baada ya kuuliwa Imam Ali (as), Waislamu walimpa baia na mkono wa utiifu Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza; hata hivyo baada tu ya kushika hatamu alikabiliwa na njama na uasi wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi kwa ajili ya kukabilina na uasi wa Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah.
Imam Hassan al Mujtaba (as) alilazimika kufanya suluhu na Muawiyah bin Abi Sufiyan kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uislamu na Waislamu. Mjukuu huyo kipenzi wa Mtume (saw) aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Benin ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa.
Wafaransa walianza kuingilia masuala ya kisiasa na kiuchumi ya Benin katika nusu ya pili ya karne ya 19 na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo mwaka 1892. Ufaransa iliendelea kuikoloni Benin hadi mwaka 1958 na hatimaye mwaka 1960 katika siku kama ya leo nchi hiyo kajipatia uhuru. ***
Katika siku kama ya leo mika 50 iliyopita, mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland.
Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani.
Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo hasa kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar'ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, Usul Fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf Iraq. Moja ya athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko mjini Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake ambayo ina vitabu zaidi laki tatu.

Miaka 20 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi.
Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Aal-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz.
Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.

Tarehe Mosi Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama.
Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi.
Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika mji wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama.
Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mama.
