Jumanne, tarehe 5 Agosti, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 11 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Agosti mwaka 2025.
Tarehe 5 Agosti mwaka 130 iliyopita, alifariki dunia Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani.
Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848.
Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Agosti 1960, nchi ya Burkina Faso iliyoko magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru.
Burkina Faso ilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa tokea katikati mwa karne ya 19. Nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Upper Volta, ilianza kujipatia mamlaka ya ndani mwaka 1958, lakini miaka miwili baadaye ilipatia uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, ilipofika mwaka 1984, nchi hiyo iliamua kubadilisha jina kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso.
Nchi hiyo ya Kiafrika inapakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Marekani, Urusi ya zamani na Uingereza ulitiwa saini.
Baada ya kuanza kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu ulikaribia kutumbukia katika vita vikubwa vya maangamizi kutokana na kuanza majaribio ya nyuklia na utengenezaji wa makombora yanayovuka mabara na yenye vichwa vya silaha za nyuklia. Suala la Cuba na kupelekwa huko makombora ya Urusi lilifikisha mgogoro huo kileleni.
Baada ya kusainiwa mkataba huo anga ya kimataifa ilitulia kidogo na kukaanza mazungumzo ya jadi kwa ajili ya kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia. Kuanzia Oktoba mwaka 1958 Marekani, Urusi na Uingereza zilitilia maanani suala la kusitisha majaribio ya silaha hizo japokuwa ziliendelea kufanya majaribio hayo.
Hatimaye na baada ya mazungumzo mapana, nchi hizo tatu zilifikia makubaliano ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 5 Oktoba mwaka 1963.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Mordad 1367 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini, mwanachuo mashuhuri na mwanamapambano wa Pakistan katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa nchi hiyo. Sayyid A'ref Husseini baada ya kupata elimu ya kidini nchini Pakistan, alifunga safari na kuelekea katika nchi za Iraq na Iran kwa shabaha ya kuongeza maarifa ya kidini. Wakati wa kutokea harakati za mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah, Allamah A'ref Husseini alikuwa hapa nchini na kuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, jambo ambalo liliukasirisha utawala wa Shah na kuamua kumfukuza nchini.

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC walipasisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu katika mkutano wa 19 wa mawaziri hao uliofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri.
Kwa mnasaba huo siku hiyo imepewa jina la 'Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu.' Azimio hilo lina utangulizi na vipengee 25. Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu lilipasishwa baada ya nchi za Kiislamu kukosoa Azimio la Haki za Binadamu lililopasishwa mwaka 1948 katika Umoja wa Mataifa ambalo lilibuniwa kwa misingi ya fikra za kiliberali za nchi za Magharibi na baadhi ya vipengee vyake vinapingana na mafundisho ya Kiislamu.
Sifa kuu inayotofautisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu na lile la Umoja wa Mataifa ni kutilia maanani haki za kiroho na kimaanawi za maisha ya mwanaadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
