Aug 15, 2025 02:25 UTC
  • Leo ni Ijumaa tarehe 15 Agosti 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Safar 1447 Hijria inayosadifiana na Agosti 15 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, mfereji wa Panama ulifunguliwa rasmi kufuatia kupita meli ya kwanza katika mfereji huo. 

Ujenzi wa mfereji huo ulianzishwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye serikali ya Marekani ilinunua kampuni ya Ufaransa iliyokuwa ikijenga mfereji huo na kukamilisha ujenzi wake.

Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic. 

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa, faqihi mkubwa na mmoja kati ya wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h.

Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, huko katikati mwa Iran, katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko Najaf, Iraq.

Akiwa huko, alipata elimu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama Allamah Mirza Shirazi na kupata daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasilatun-Najat” na “Tanbihul-Ummah wa Tanzihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.   

Miaka 78 iliyopita India ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza, baada ya miaka mingi ya mapambano ya kupigania uhuru.

India ina historia kongwe na watawala mbalimbali wa ndani na nje wamewahi kutawala nchini humo.

Mapambano ya wananchi wa India dhidi ya mkoloni Muingereza yalipamba moto zaidi baada ya kuasisiwa Chama cha Congress ya Kitaifa na kujiunga na chama hicho Mahatma Gandhi.     

Miaka 77 iliyopita, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea.

Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini. 

Miaka 65 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola.  

Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola.       

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 24 Mordad 1369 Hijria Shamsia, Saddam Hussein Rais wa zamani wa Iraq alimtumia barua Hujjatul Islam Walmuslimin Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, akimjulisha kwamba amekubali kikamilifu vipengee vya makubaliano ya mpaka yaliyotiwa saini 1975 nchini Algeria.

Hata hivyo, tarehe 27 Shahrivar 1359 Hijria Shamsia, Saddam Hussein baada ya kushawishiwa na madola ya kibeberu ya Magharibi, alijitokeza kwenye televisheni ya Iraq na kuuchanachana mkataba huo, na baada ya siku chache, alianza kuivamia ardhi ya Iran.

Saddam Hussein na waitifaki wake walidhani kwamba, muda mfupi tu baada ya kuivamia ardhi ya Iran wangeliweza kuuangusha mfumo mchanga wa Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo kusimama kidete wananchi na mapambano ya wapiganaji shupavu wa Kiislamu wa Iran yalibatilisha njama zao na jeshi vamizi la Iraq likalazimika kurejea nje ya mipaka ya Iran baada ya kushindwa mtawalia. 

Na siku kama hii ya leo miaka 20 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Agosti 2005, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967, baada ya kutokea vita vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini pamoja na hayo utawala huo katili hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya Gaza na kuwaua Wapalestina wengi hasa  wanawake na watoto.