Ijumaa, tarehe 29 Agosti, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 5 Mfunguo Sita Rabiul Awwal, mwaka 1447 Hijria, inayosadifiana na tarehe 29 Agosti mwaka 2028.
Siku kama ya leo miaka 179 iliyopita Dar al-Fonon", chuo kikuu cha kwanza cha Iran cha mtindo wa kisasa, kilifunguliwa. Chuo hicho kilianzishwa mwanzoni mwa utawala wa Nasser al-Din Shah Qajar, kupitia juhudi za Mirza Taghi Khan Amir Kabir, kansela aliyekuwa na busara.
Madhumuni ya kuanzishwa chuo hicho ilikuwa kupata taaluma za tasnia na sayansi mpya za zama hizo.
Katika miaka mingi ya uendeshaji wake, chuo hicho kilikuwa na wahitimu wengi, ambao baadhi yao walipata vyeo vya juu serikalini.
Kuanzishwa kwa kituo hiki cha kitamaduni kunatambuliwa kuwa hatua ya mabadiliko katika historia ya elimu ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita Urusi ya zamani ilifanya majaribio ya siri ya bomu lake la kwanza la nyuklia.
Kwa utaratibu huo Urusi ikawa nchi ya pili yenye mabomu ya nyuklia baada ya Marekani suala ambalo liliibua mlingano wa nguvu kati ya nchi hizo mbili ambao ulipewa jina la “Mlingano wa Hofu.” Kwani katika hali hiyo kila mmoja wao aliogopa kutumia silaha hizo za nyuklia dhidi ya mwenzake kwa kuogopa kushambuliwa pia na silaha kama hizo.
Tangu wakati huo Marekani na Urusi ya zamani ziliingia katika vita vya kipropaganda. Vita hivyo vilipewa jina la "Vita Baridi" au Cold War kwa kimombo. Vita hivyo vya kati ya kambi ya Mashariki na Magharibi viliendelea hadi wakati wa kusambaratika Urusi ya zamani mwaka 1991.

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, msanii na mchoraji maarufu wa katuni wa Palestina, Naji al Ali, ambaye alikuwa ameshambuliwa na maajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD huko London, Uingereza alifariki dunia baada ya siku 38 za kuwa katika hali ya kupoteza fahamu.
Al-Ali alizaliwa mwaka 1937 huko Palestina na alilazimika kukimbia nchi yake akiwa bado mtoto akiwa pamoja na familia yake na kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Ain al-Halwa kusini mwa Lebanon kutokana na ukatili na unyama wa Wazayuni. Alishuhudia kwa karibu mashaka na masaibu ya Wapalestina na akaamua kutumia kipawa chake cha usanii kufichua unyama na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia sanaa ya uchoraji vibonzo.
Hatimaye magaidi wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD walimshambulia na kumuua mwanamapambano huyo akiwa njiani kuelekea ofisini kwake mjini London. Miezi sita baada ya kufariki kwake dunia Jumuiya ya Kimataifa ya Wachapishaji ilimtunuku msanii huyo tuzo ya Kalamu ya Dhahabu ya Uhuru.

Na Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar'ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96.
Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, Usul Fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf Iraq.
Moja ya athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar'ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko katika mji wa Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake duniani.
