Sep 04, 2025 02:32 UTC
  • Alkhamisi, 4 Septemba, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria, sawa na tarehe 4 Septemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Agha Bozorge Tehrani.

Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini.

Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu.Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.   

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, mota ya kwanza ya umeme ilitengenezwa.

Mvumbuzi na mtengenezaji wa mota hiyo alikuwa Thomas Edison mtaalamu na mtafiti wa Kimarekani. Kwa kutumia mota hiyo ya umeme, Edison alianzisha kiwanda cha umeme katika mji wa New York na wakati huo huo akawa amefanikiwa kudhamini sehemu ya mahitaji ya mwanga katika mji huo. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba, mwaka 1879, Edison alifanikiwa kuvumbua balbu.   

Tarehe 4 Septemba miaka 117 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Richard Wright.

Baada ya mashaka makubwa maishani, Richard Nathaniel Wright alianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 30. Baadhi ya vitabu vyake vinaakisi sehemu ya maisha ya kifukara na ya kuchosha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Ameandika vitabu vingi kama Black Boy, Native Son, Uncle Tom's Children na The Outsider.   

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin.

Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 Miladia katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland.

Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa.   

Na tarehe 13 Shahrivar miaka 47 iliyopita kulifanyika maandamano ya kwanza ya mamilioni ya Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Maandamano hayo yalianza baada ya Swala ya Eid-ul-Fitr kutoka sehemu nne za Tehran. Waandamanaji waliokuwa wamebeba picha kubwa ya Imam Ruhullah Khomeini (RA), kiongozi wa hayati wa Mapinduzi ya Kiislamu, walipaza sauti na nara za kudai uhuru, kujitawala na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.

Maandamano hayo makubwa ya mamilioni, ambayo yalikuwa msingi wa maandamano ya kihistoria ya tarehe 17 Shahrivar ya mwaka huo huo, yalimalizika baada ya Sala ya jamaa ya adhuhuri.