Jumamosi, 20 Septemba, 2025
Leo ni Jumamosi 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na 20 Septemba 2025 Miladia.
Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1084 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man nchini Syria. Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Halab (Aleppo). Baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30 na kwenda kwa kasi ndogo na lilitengenezwa na Gordon Branz, raia wa Uingereza. Hii leo mabasi bora na ya kisasa ni miongoni mwa vyombo muhimu vya usafiri kote duniani.

Katika siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria, na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Tarehe 20 Septemba miaka 46 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Bokasa alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake, David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Na siku kama ya leo, miaka 14 iliyopita, aliuawa Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama nchini Afghanistan, Burhanuddin Rabbani. Alizaliwa tarehe 20 Septemba mwaka 1940. Alikuwa kiongozi wa chama cha Jumuiya ya Kiislamu nchini humo na rais rasmi wa kwanza wa utawala wa Mujahidina huko Afghanistan. Hadi mwisho wa maisha yake, Burhanuddin Rabbani alikuwa mkuu wa Baraza Kuu la Usalama lililoundwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Hamid Karzai. Baraza hilo lilikuwa na wadhifa wa kufanya mazungumzo na kundi la Taleban kwa lengo la kufikiwa suluhu na kumaliza mgogoro wa taifa hilo kwa njia ya amani. Rabani aliuawa katika siku kama ya leo na gaidi aliyekuwa ameficha bomu katika kilemba chake, wakati alipoingia ofisini kwa mwanasiasa huyo kwa madai ya kufanya mazungumzo.
