Ijumaa, Septemba 26, 2025
Leo ni Ijumaa mwezi Tatu Mfunguo Saba Rabiu Thani 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Septemba 2025 Milaadia.
Miaka 155 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1292 Hijiria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Qasim Kalantari. Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu wa Tehran. Ayatullah Kalantari alibobea sana katika elimu za hadithi, falsafa na mantiki. Msomi huyo alipata elimu kwa wasomi mashuhuri wa mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq akiwemo Shekh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya Ijtihad. Ameandika vitabu vingi hasa katika uwanja wa fiqhi na sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.

Katika siku kama ya leo miaka 137 iliyopita alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.
Siku kama hii ya leo miaka 13 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus wakitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita yaani Septemba 26, 1959 Milaadia, "S. W. R. D. Bandaranaike" (Solomon West Ridgeway Dias Bandaranaike), Waziri Mkuu wa wakati huo wa Sri Lanka, aliualiwa na kuhani mmoja wa Kibudha. Bandaranaike alihitimu masomo ya Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, na alianzisha "Shirika la Uhuru wa Milioni la Sri Lanka" mwaka wa 1952 Milaadia. Kwa maneno yake mwenyewe Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Sri Lank alikiri kwamba alipata ujasiri kutoka kwa Dk Mossadegh wa nchini Iran. Ni wataalamu, wafanyakazi, wakulima na walimu pekee ndio walioruhhusiwa kujiunga na chama chake. Milango ya chama ilifungwa kwa makabaila, wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na matajiri. Kisha aliunda muungano na vyama vinne vya kisoshalisti na demokrasia ya kijamii na akashinda uchaguzi mwaka wa 1956 na kuwa Waziri Mkuu na kauli mbiu "Sri Lanka ni ya Sri Lanka na lugha rasmi ya nchi inapaswa kuwa lugha ya asili." Bandaranaike alitimiza ahadi zake zote za uchaguzi na kufuta lugha ya Kiingereza, urithi wa ukoloni wa Uingereza, na kufuata sera ya taifa huru na kuanzisha uhusiano na baadhi ya nchi za kikomunisti. Hata hivyo, tarehe 25 Septemba 1959, Bandaranaike alipigwa risasi huko Colombo na akafa siku iliyofuata kutokana na majeraha. Baada ya kuuawa kwa Bandaranaike, hisia za wananchi zilizuka na kumtaka mkewe Sirima ambaye hakuwa na uzoefu wa masuala ya siasa wala serikali achukue nafasi yake. Sirima, waziri mkuu wa kwanza mwanamke duniani, alihudumu kwa mihula mitatu mfululizo ya waziri mkuu wa Sri Lanka hadi kifo chake mwaka 2000. Wakati huo huo, chama cha Million Freedom Party na vyama mbalimbali vya Sri Lanka vilimchagua bintiye Bandaranaike, Chandrika Kumaratunga, kuwa rais mwaka 1994, na kuanzia mwaka huo hadi 2000, binti huyo alikuwa rais na mama yake alikuwa waziri mkuu.