Nov 09, 2025 02:34 UTC
  • Jumapili, 9 Novemba, 2025

Leo ni Jumapili 18 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 9 Novemba 2025 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1119 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Athari yake mashuhuri ni kitabu cha Al Iqdul-Farid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi. 

Abdu Rabbuh

 

Miaka 997 iliiyopita katika siku kama ya leo, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa lakabu ya Najashi aliaga dunia huko Samarra Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najashi alikuwa alimu na msomi mashuhuri katika karne ya tano Hijria na alikuwa amebobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. 

Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa lakabu ya Najashi

 

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, alizaliwa Ivan Turgenev mwandishi mashuhuri wa riwaya wa Russia. Turgenev alisomea fasihi ambapo vitabu vyake vingi vilitetea sana uhuru na haki za wanavijiji. ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alisumbuliwa na utawala wa Kitzar wa Urusi na kuulazimika kuhama na kuuelekea Ufaransa.

Ivan Turgenev

 

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahori mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahori alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana na shairi lake la kwanza alilipa jina la 'Naleh Yatiim' kwa maana ya kilio cha yatima. Allama Iqbal Lahori alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allamah Muhammad Iqbal alifariki dunia mwaka 1938. 

Allama Muhammad Iqbal Lahori

 

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abdul Aziz bin Saud mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia na mwasisi wa utawala wa Aal Saud. Abdul Aziz bin Saud ambaye ni mwasisi wa utawala wa kifamilia wa Saudi Arabia, alizaliwa tarehe 15 Mei 1880. Mtawala huyo alikuwa kibaraka wa Uingereza na tangu awali alikuwa na tamaa ya kutawala nchini Saudi Arabia hususan katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina.

Abdul Aziz bin Saud

 

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, nchi ya Cambodia ilijikomboa kutoka kwenye makucha ya mkoloni Mfaransa na kujitangazia uhuru. Kijiografia Cambodia ipo kusini mashariki mwa Asia. Akthari ya wananchi wa Cambodia ni wa jamii ya Khmer na wanazungumza lugha ya Kikhmeri. Kuanzia karne ya 8 hadi 13 Miladia, Cambodia ilikuwa nchi yenye nguvu ambapo mbali na ardhi ya sasa ya nchi hiyo, sehemu kubwa ya ardhi ya Thailand, Laos na Vietnam ilikuwa katika udhibiti wa nchi hiyo. 

 

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Charles de Gaulle mwanajeshi, mwanasiasa mashuhuri na rais wa zamani wa Ufaransa aliaga dunia. Jenerali Charles André Joseph Marie de Gaulle alizaliwa Novemba 22 mwaka 1890 katika mji wa Lille. Mwaka 1940 aliteuliwa kuwa jenerali kijana zaidi katika Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa. Baada ya majeshi ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani katika vita, Charles de Guelle alikimbilia Uingereza na kuongoza harakati za mapambano ya Ufaransa. 

Charles de Gaulle

 

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, Sheikh Nusratullah Ansari mwanamapambano wa kimapinduzi wa Iran alikufa shahidi kutokana na mateso ya makachero wa Shirika la Usalama wa Taifa la utawala wa Shah lililojulikana kwa jina la SAVAK. Hujjatul Islam Nusratullah Ansari alizaliwa huko Buin Zahra. Sambamba na masomo yake ya Hawza alikuwa akiendesha pia harakati za mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah nchini Iran. Hatimaye alitiwa mbaroni mwaka 1354 Hijria Shamsia na kufa shahidi katika siku kama ya leo baada ya miezi sita ya mateso. 

Sheikh Nusratullah Ansari

 

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, ukuta wa Berlin ambao ulikuwa ukiugawa mji huo katika sehemu mbili za mashariki na magharibi kwa kipindi cha miaka 28 hatimaye ulivunjwa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa mji huo lilikuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku eneo la magharibi likidhibitiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Machafuko yaliyotokea mjini Berlin hapo mwaka 1961 na wakazi wa mashariki kukimbilia upande wa magharibi, kulizitia wasiwasi serikali za Urusi ya zamani na Ujerumani Mashariki, suala lililozipelekea nchi hizo kujenga ukuta huo ambao baadaye uliokana kuwa nembo ya kuwaganywa Ujerumani. Hata hivyo kuporomoka kwa Urusi ya zamani ambako kuliacha taathira kubwa katika tawala za kikomunisti za Ulaya Mashariki kulipelekea kuvunjwa ukuta huo wa Berlin hapo mwaka 1989.