Jumanne, Novemba 25, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 4 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria mwafaka na 25 Novemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa.
Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo.
Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba.

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini.
Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah.
Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya uwagaji damu.
Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30.
Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.

Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi.
Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic.

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita alifariki dunia Vasiliy Ivanovich Alekseyev, bingwa mnyanyuaji uzani wa nchini Russia na kimataifa.
Alekseyev alipata ushindi mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani na mwaka 1976 Montréa, Canada kwa kujinyakulia medali za dhahabu. Katika kipindi cha ushindi wake, Vasiliy Ivanovich Alekseyev aliweka rekodi ya dunia. Alikuwa mnyanyuaji uzani ambaye aliweza kuweka rekodi ya kunyanyua kilogramu 645 kwa kupindukia kilogramu 600.
Mwaka 1993 Shirikisho la wanyanyuaji uzani duniani lilimteua Alekseyev kuwa mmoja wa mabingwa wakubwa katika fani hiyo. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 nchini Ujerumani kutokana na matatizo ya moyo.

Na katika siku kama hii ya leo miaka 9 iliyopita alifariki dunia Fidel Castro, ambaye jina lake kamili ni Fidel Alejandro Castro Ruz, kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba.
Alizaliwa tarehe 13 Agosti 1926 katika eneo la Biran na kumaliza masomo yake katika Kitengo cha Sheria ya Chuo Kikuu cha Havana. Castro alianzisha harakati za kisiasa mwaka 1947 akiwa bado mwanafunzi wa chuo kikuu.
Castro alikuwa miongoni mwa nembo kuu za mapinduzi ya kikomunisti katika kanda ya Amerika ya Kusini. Wakati wa utawala wake nchini Cuba, viwanda na biashara vilitaifishwa na mageuzi ya serikali ya ujamaa yalitekelezwa katika jamii nzima ya nchi hiyo.
Fidel Castro pia alikuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) kwa mihula miwili. Castro alifariki asubuhi ya Jumamosi, Novemba 26, 2016 kutokana na ugonjwa na uzee akiwa na umri wa miaka 90.
