Alkhamisi, Novemba 27, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Novemba 2025.
Tarehe 27 Novemba miaka 106 iliyopita iliainishwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Baada ya kumalizika vita hivyo na kutiwa saini mkataba wa amani wa Versailles kulisainiwa mikataba mingine kadhaa ya kuainisha mustakabali wa tawala za Austria na Hungary na utawala wa Othmania na nchi ya Bulgaria ambayo kila mmoja ulikuwa na masharti mazito na kutoa fidia nchi hizo kwa zile zilizopata ushindi.
Kuainishwa kwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati katika mkutano wa Paris kulibadili kikamilifu ramani ya dunia.

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo.
Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani.
Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti.

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Eugene O’Neill mwandishi Kimarekani.
Eugene O’Neill ambaye alikuwa mashuhuri pia katika uandishi wa tamthilia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 65. Alizaliwa mwaka 1888 na maisha yake yalitawaliwa na matukio mengi. Eugene O’Neill alikuwa na mapenzi makubwa na tamthilia na ndio maana akapewa jina la mtoto wa tamthilia.
Mwaka 1936 Eugene O'Neill alitunukiwa tuzo ya Nobel. Baadhi ya vitabu vya mwandishi huyu ni Mfalme Jones, The First Man na Days Without Ends.

Katika siku kama hii ya leo miaka 30 iliyopita aliaga dunia Dkt. Sayyid Sadeq Goharin, mwandishi maarufu wa fasihi na mtafiti wa taaluma ya Irfani ya Kiislamu.
Baada ya kukamilisha masomo yake ya juu alianza kufundisha katika shule za upili, akiendelea na masomo yake katika shahada ya uzamivu kwenye taaluma ya fasihi ya Kiajemi; na ni wakati huu ndipo alipoandika kitabu cha "Dictionary of Words and Interpretations of the Mathnavi" katika juzuu 9 kama tasnifu yake.
Katika risala hii, ambayo labda ndio kazi yake muhimu na ya kina zaidi, Profesa Goharin ameeleza msamiati, istilahi, tafsiri za fumbo, sitiari, istilahi za Qur'ani, na Hadithi, n.k., ambazo zinaonekana katika kitabu cha Masnavi Maanavi cha Jalaluddin Rumi.
Baadhi ya kazi zake zingine ni pamoja na: Pire Jangi, Hadithi ya Bahram Goor, Maelezo ya Istilahi za Kisufi, na Sheikh San'an.
