Dec 06, 2025 02:43 UTC
  • Jumamosi, 06 Disemba, 2025

Leo ni Jumamosi mwezi 15 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria sawa na 6 Disemba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1411 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilitokea vita vya Jamal baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu. 

 

Tarehe 15 Jamadithani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 676 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.

 

Katika siku kama ya leo miaka 247 iliyopita yaani tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa. Gay-Lussac alifanya tafiti nyingi na kugundua vitu mbalimbali katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa mambo yaliyogunduliwa na mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya. Miongoni mwa kazi zake muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850. 

 

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, alikufa shahidi rubani Ahmad Keshvari. Brigedia Ahmad Keshvari aliingia katika Jeshi la Anga la Iran mwaka 1351 Hijria Shamsia na kuhitimu mafunzo ya kuendesha helikopta. Baada ya ushindi wa Mapindizi ya Kiislamu nchini mwaka 1979 alitoa mchango mkubwa katika kupambana na makundi yaliyokuwa dhidi ya Mapinduzi katika maeneo ya magharibi mwa Iran na baadaye kidogo aliteuliwa kuwa kamanda wa Jeshi la Anga katika eneo la Ilam. Baada ya jeshi la Saddam Hussein kuvamia ardhi ya Iran, Brigedia Keshvari alikuwa mstari wa mbele kupambana na jeshi la adui na kulisababishia hasara kubwa ya nafsi na mali. Ahmad Keshvari aliuawa shahidi baada ya kukamilisha operesheni iliyokuwa na mafanikio akiwa njiani kurejea nchini.  

 

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Manouchehr Jahan Beglu, profesa wa miziki ya kiasili ya Kiirani akiwa na umri wa mia 62. Profesa Jahan Beglu alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsia Mwanamuziki huyo wa miziki ya kiasili alijifunza sanaa ya muziki kutoka kwa wasomi wakubwa wa tasnia hiyo na kisha akaelekea Austria na kupata shahada ya juu zaidi katika fani hiyo. Alirudi nchini na kuwasaidia wanafunzi wengi kufanya utafiti na kukuza tasnia hiyo. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwenye jimbo la Uttar Pradesh nchini India. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Zahiruddin Muhammad Babur juu ya kilima na tangu wakati huo ulijulikana kwa jina la Msikiti wa Babri. Baada ya kupita karne tatu tangu ujengwe yaani mwaka 1855, mtawala mmoja Muingereza alipotosha ukweli kwa makusudi na kuandika kuwa msikiti huo umejengwa kwenye magofu ya jumba la ibada ya masanamu la Wahindu. Suala hilo lilikuwa chanzo cha fitina na ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wahindu. Mwaka 1992 Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka walivamia Msikiti wa Babri na kuubomoa kikamilifu, suala ambalo lilizusha vita baina ya Waislamu na Wahindu.