Dec 07, 2025 02:26 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili mwezi 16 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria sawa na 7 Disemba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1026 iliyopita, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mashuhuri wa Andalusia. Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa chanzo cha kuaminika kinachoonyesha matukio ya wakati huo ya Uhispania.

 

Tarehe 7 Disemba miaka 136 iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani  lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929. 

 

Miaka 84 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl (Pearl Harbor). Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilipokuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ilitangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia.

 

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah. Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Muswaddeq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo". 

 

Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Abdul Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni.