Jumamosi, 13 Disemba, 2025
Leo ni Jumamosi mwezi 22 Mfunguo Tisa 1447 Hijria mwafaka na 13 Disemba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa mashairi wa Kiislamu kwa jina la Ibn Hajjaj. Ibn Hajjaj alizaliwa mjini Baghdad, Iraq na alijikita katika taaluma ya mashairi akiwa bado kijana na kutokea kuwa maarufu katika uwanja huo. Alitunga mashairi mengi yanayowaenzi na kuwasifu Ahlul bait wa Mtume (saw) na kuwashambulia wapiznani wa Uislamu na Mtume. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi yenye juzuu kumi inayohifadhiwa katika maktaba mbalimbali duniani.

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita alifariki dunia mmoja wa maraaji' wakubwa wa Kiislamu, Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti. Katika uhai wake alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya masomo ya dini na kuhudhuria masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti taratibu akawa mmoja wa maraaji' wakubwa katika mji mtakatifu wa Najaf. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kiitwacho Badaiul Afkar.

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, Majlisi ya Waasisi nchini Iran ambayo iliundwa kwa ajili ya kuhamisha mfumo wa kisultani kutoka silsila ya Qajar hadi utawala wa kifalme wa Pahlavi, ilitekeleza kazi yake kwa kufanya mabadiliko ya kimsingi katika Katiba ya Iran. Kwa msingi huo utawala wa miaka 153 wa wafalme wa Kiqajari nchini Iran ulifikia kikomo na badala yake ukaanza utawala wa miaka 53 wa Pahlavi hapa nchini.

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita sawa na Disemba 13 mwaka 1931, aliaga dunia Gustave Le Bon mwanafikira wa masuala ya mashariki na mwandishi mtajika wa Kifaransa. Gustave Le Bon mwanafikra na mwandishi wa Kifaransa aliyekuwa amebobea katika historia ya utamaduni wa Kiislamu alizaliwa mwaka 1841 nchini Ufaransa. Gustave alianza kusoma masomo ya utabibu baada ya kukamilisha masomo ya awali hata hivyo kile kilichompelekea kuwa maarufu ni utafiti wa kihistoria na kijamii alioufanya. Hii ni kwa sababu alikuwa na hamu ya kujifunza saikolojia ya jamii mbalimbali, kuendeleza na kukamilisha nadharia ya saikolojia ya jamii. Gustave Le Bon kimsingi alifanya utafiti wake wake wa kijamii kuhusu masuala ya saikolojia ambapo aliandika vitabu vingi katika uwanja huo; vitabu ambavyo viliungwa mkono na wanafikra kutoka nchi mbalimbali na kufasiriwa katika lugha tofauti. Hatimaye Dakta Gustave Le Bon aliaga dunia tarehe 13 mwezi Disemba mwaka 1931 karibu na Paris akiwa na umri wa miaka 90.

Tarehe 13 mwezi Disemba mwaka 1963 yaani miaka 62 iliyopita, Sheikh Mahmood Shaltoot, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar na Mufti Mkuu wa zamani wa Misri aliaga dunia. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Misri alizaliwa mwaka 1892 nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 14 alianza masomo ya shule ya upili katika Chuo cha Kidini cha Alexandria kilichokuwa tawi la Al Azhar. Alipata chetu cha chuo kikuu mwaka 1918 na kuanza kufunza katika chuo hicho hicho na hatimaye akahamia chuo kikuu cha al Azhar mwaka 1927. Alizidi kupanda cheo kielimu na kuteuliwa kuwa mwanachama wa Baraza la Fatwa chuoni hapo. Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar ambapo alitoa huduma kubwa. Kati ya hatua muhimu zilizochukuliwa na Sheikh Shaltoot katika kipindi cha uongozi wake ni jitihada za kuimarisha umoja na mshikamano kati ya madhehebu za Kiislamu. Baada ya kuandikiana barua kadhaa na Ayatulahil Udhma Borujerdi aliyekuwa marjaa na kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Sheikh Shaltut alitambua rasmi madhehebu ya Shia Ithnaashari. Aliamrisha madhehebu ya Shia yafunzwe katika Chuo Kikuu cha Al Azhar sawa na madhehebu zingine za Kiislamu. Aidha alitoa fatwa mashuhuri na kusema kuwa, inajuzu kwa Mwislamu yeyote kufuata madhehebu ya Shia Jaafariya. Sheikh Shaltoot aliaga dunia mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 72.

Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo dikteta wa zamani wa Iraq alitiwa mbaroni akiwa katika maficho yake karibu na Tikrit huko kaskazini mwa Baghdad. Saddam alijificha katika eneo hilo baada ya Iraq kuvamiwa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwezi Machi 2003. Kutiwa nguvuni dikteta huyo wa Iraq aliyemwaga damu za raia wengi wa nchi hiyo kuliwafurahisha sana Wairaki na nchi kama vile Iran na Kuwait ambazo zimepatwa na maafa makubwa kutokana na udhalimu za Saddam Hussein dhidi ya nchi hizo. Katika upande mwingine, pamoja na kuwa walimwengu walikuwa wakisubiri kwa hamu kusikia jinai zilizotendwa na dikteta huyo wa zamani wa Iraq wakati wa utawala wake, Marekani ilimweka dikteta huyo chini ya uangalizi wake baada ya kumtia nguvuni lengo likiwa ni kuzuia kufichuliwa ushirikiano wa karibu uliokuwapo kati ya dikteta huyo na nchi za Magharibi hususan ikulu ya Rais wa Marekani, White House.
