Jan 02, 2026 02:32 UTC
  • Ijumaa, Januari 2, 2026

leo ni Ijumaa tarehe 12 Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe Pili Januari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1415 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume (saw) na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi.

Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka.

Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.

Katika siku kama hii ya leo miaka  1241 iliyopita aliaga dunia Abu Hudhayfah, mpokezi wa Hadith, habari za kihistoria na visa vya Mitume.

Aliishi kwa muda katika miji ya Makka na Madina na akajishughulisha na kujifunza Hadith.

Abu Hudhayfah alikuwa mpokezi wa kutegemewa wa Hadith. Moja ya vitabu vyake muhimu ni "Al-Mubtada", ambacho kinahusu kuumbwa kwa mwanadamu na visa vya manabii. Kazi nyingine muhimu ya Abu Hudhayfah ni maelezo ya riwaya ya Imam Ja'far al-Sadiq (AS) kuhusu safari ya Mi'raji ya Mtume Muhammad (SAW).   

Siku kama hii ya leo miaka 181 posta ya kwanza yenye muundo wa kisasa ilifunguliwa huko Vienna mji mkuu wa Austria.

Kabla ya kuanzishwa chombo makhsusi kwa ajili ya kusafirisha barua na vifurushi vya posta, mizigo hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwa kutumia farasi, ngamia au boti makhsusi. Hata hivyo miaka mingi baadaye kulibuniwa mbinu mpya na mfumo wa posta ukaboreshwa zaidi na kuwa na sura ya sasa.   ****

Katika siku kama ya leo miaka 160 iliyopita leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia.

Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford.

Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'.

Katika siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia.

Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana.

Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii.   

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 2 Januari 1971, washabiki wa soka wasiopungua 66 nchini Scotland walifariki dunia baada ya kuanguka uzio wa uwanja wa Ibrox Park mjini Glasgow.

Watu wengine zaidi ya 200 walijeruhiwa. Maafa hayo yalitokea wakati wa kuchezwa mechi kati ya mahasimu wawili wakuu wa soka nchini humo, klabu ya Celtic na Rangers.    ****

Katika siku kama ya leo miaka 10 iliyopita yaani tarehe Pili Januari 2016 utawala wa Saudi Arabia ulimuua mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al-Nimr. 

Baqir al Nimr aliyekuwa mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia alizaliwa tarehe 21 Juni mwaka 1959 katika mji wa Awwamiyya huko mashariki mwa Saudi Arabia. Alipata elimu ya msingi katika mji huo na mwaka 1400 Hijria yaani mwaka 1989 alielekea Tehran nchini Iran na kupata elimu katika chuo cha kidini cha Qaim kilichoasisiwa na Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi. Baada ya kupata elimu katika chuo hicho kwa kipindi cha miaka 10 Sheikh Nimr alikwenda Syria na kuendelea kutafuta elimu zaidi katika Chuo cha Kidini cha Bibi Zainab (as).

Aliporejea Saudi Arabia, Sheikh Nimr aliasisi kituo cha kidini cha al Imam al Qaim katika mji wa Awwamiyya ambacho kiliweka jiwe la msingi la kuanzishwa Kitiuo cha Kiislamu hapo mwaka 2011.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu daima alikuwa akikosoa siasa za ukandamizaji na kibaguzi za utawala wa kifalme wa Saudia na alifungwa jela mara kadhaa kutokana na kusema haki na kweli.

Mara ya mwisho Sheikh Baqir Nimr alikamatwa tarehe 8 Julai mwaka 2012 katika maandamano makubwa ya Waislamu wa Kishia ya kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud na tarehe 15 Oktoba msomi huyo wa Kiislamu alihukumiwa kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo.

Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016. Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu.   

Na miaka 6 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Muhammad Taqi Mesbah Yazdi, faqihi, mfasiri wa Qur'ani na profesa wa chuo kikuu cha Qum nchini Iran.

Allamah Misbah Yazdi alianzisha Taasisi ya Utafiti wa Kisayansi ya Baqirul Uloom, na kisha Taasisi ya Utafiti ya Imam Khomeini huko Qum. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alishika nyadhifa nyingi ikiwa ni pamoja na mwakilishi wa watu wa Mkoa wa Khorasan katika Baraza la Wataalamu, mjumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni, mjumbe wa Jumuiya ya Maprofesa wa Semina ya Qum, na rais wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt.

Miongoni mwa kazi zake, tunaweza kutaja kitabu cha Maarifa ya Qur'ani chenye juzuu 9 na pia Mafunzo ya Falsafa katika juzuu mbili.