Alkhamisi, 29 Januari, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Sha'ban, 1447 Hijria sawa na tarehe 29 Januari, 2026.
Siku kama ya leo miaka 966 iliyopita sawa na tarehe 9 Sha'ban mwaka 481 Hijria, aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri.
Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa, kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi.
Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo. ****
Katika siku kama ya leo miaka 870 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Abul Barakaat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Anbari fakihi na mtaalamu mashuhuri wa lugha wa mjini Baghdad.
Alihitimu masomo yake katika Chuo cha Nidhamiyyah mjini Baghdad na kutokana na kupata alama za juu mno katika masomo alianza kufundisha katika chuo hicho. Ibn Anbari hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa. ****
Miaka 289 iliyopita, mnamo Januari 29, 1737 alizaliwa Thomas Paine, mwanasiasa na mwandishi mwanamapinduzi wa Uingereza.
Baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya kati Paine aliamua kujishughulisha na kazi mbalimbali lakini hakufanikiwa katika yoyote kati ya hizo.
Hatimaye mnamo mwaka 1774, yaani mwaka mmoja kabla ya kuanza vita vya uhuru wa Marekani aliwasili nchini humo na kuanza kazi ya uandishi. Tasnifu yake iliyoitwa "Akili Timamu" iliwaathiri mno wananchi na viongozi wa Marekani na kuimarisha azma yao ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Uingereza. Baada ya uhuru wa Marekani, Thomas Paine alirejea kwao Uingereza ambako aliandika kitabu "Haki za Mtu" kutetea Mapinduzi ya Ufaransa.
Kwa sababu huko Uingereza alitambuliwa kama haini, Paine alilazimika kuelekea Ufaransa ambako alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Taifa. Alifia Marekani mwaka 1809 katika hali ya simanzi na ufakiri. ***
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita Mfalme Faisal wa Kwanza, mtoto wa Hussein Bin Ali Sharif wa mjini Makkah aliteuliwa kuwa mfalme wa Iraq katika mazingira yaliyoandaliwa na Uingereza.
Katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Uingereza ilimuahidi Sharif wa Makkah kuwa mtawala wa Hijazi endapo angekubali kupambana na mtawala wa dola la Othmania ambaye alikuwa ameungana na Ujerumani. Hata hivyo kinyume na ahadi yake, London ilimuwekak madarakani Abdul Aziz bin Saud kutawala ardhi ya Hijazi. Uingereza ilichukua hatua hiyo baada ya kuona kuwa, misimamo ya Abdul Aziz ambayo ni ya Uwahabi, ilikuwa inakubaliana sana na sera zake za kuwagawa Waislamu na hatimaye kuwatala.
Katika kujaribu kumbembeleza Hussein Bin Ali Sharif, London ilimteua mtoto wake wa kiume aliyeitwa Faisal wa Kwanza na kumpa uongozi wa Syria. Hata hivyo Ufaransa iliyokuwa imeikalia kwa mabavu Syria ilipinga uteuzi huo na hivyo ikaamua kumfukuza kutoka Syria. Baada ya hapo London ilimteua tena Faisal wa Kwanza kuwa mtawala wa Iraq ambayo wakati huo, ilikuwa koloni lake. Faisal wa Kwanza aliendelea kuwa kiongozi nchini humo hadi mwaka 1933 ambapo alifariki dunia. Katika kipindi chote cha utawala wake alikuwa akitumikia maslahi ya mkoloni Mwingereza. ********
Miaka 100 iliyopita, mnamo tarehe 29 Januari 1926, alizaliwa Profesa Muhammad Abdussalam, mwanafizikia mbobezi wa Pakistan katika mji wa Punjab mashariki ya nchi hiyo.
Abdussalam, ambaye alizaliwa katika familia ya kidini alianza kudhihirisha mapema kipawa kikubwa alichokuwa nacho kwa kufanikiwa kuingia chuo kikuu cha Punjab akiwa na umri wa miaka 14. Na baada ya kuhitimu shahada ya pili ya Uzamili akiwa na umri wa miaka 20 alielekea chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza ya Hisabati na Fizikia, mwaka 1951, Abdussalam alihitimu shahada yake ya Uzamivu au PhD ya Fizikia na kutunukiwa tuzo ya Adams.
Mwaka 1979, Profesa Muhammad Abdussalam pamoja na watafiti wengine wawili, alitunikiwa tuzo ya amani ya Nobeli na kuwa mwanasayansi wa kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu kushinda tuzo hiyo. Mwanasayansi huyo aliteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya sayansi na elimu wa rais wa Pakistan kuanzia mwaka 1961 hadi 1974. Katika uhai wake, Muhammad Abdussalam alivumbua vitu kadhaa wa kadhaa na aliaga dunia mwaka 1996. ****
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, yaani tarehe 29 Januari mwaka 1963, alifariki dunia mshairi wa Kimarekani Robert Frost.
Malenga huyo alizaliwa mwaka 1874. Kipaji chake kikubwa katika sanaa ya mashairi kilimuwezesha kuandika diwani yake ya kwanza ya mashairi akiwa na umri wa miaka 20.
Frost aliipa diwani hiyo ya mashairi jina la "A Boy's Will". Malenga huyo mara kadhaa alitunukiwa tuzo ya usanii ya Pulitzer. ***
Tarehe 9 Bahman miaka 47 iliyopita watu wengi wa mji wa Tehran walielekea katika msikiti wa chuo Kikuu cha Tehran, baada ya wanaharakati wa kidini kukusanyika katika chuo hicho wakipinga hatua ya utawala wa Shah ya kumzuia Imam Khomeini (M.A) kurejea hapa nchini. Watu waliandamana katika miji mingine ya Iran kupinga hatua hiyo, na kutaka kupinduliwa utawala wa kidhulma wa Shah na kurejea Imam Khomeini (M.A) hapa nchini. Siku hiyo wanajeshi wa utawala wa Shah kwa mara nyingine waliwashambulia wananchi, kujeruhi na kuua shahidi Waislamu wengi miongoni mwao. ***