Feb 08, 2026 02:21 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili 19 Shaaban 1447 Hijria mwafaka na 8 Februari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, kulijiri vita vya Bani Mustaliq.  Bani Mustaliq ni moja ya koo za kabila la Khuza'a ambao uliohamia katika viunga vya mji wa Makka, muda mrefu katika historia. Viongozi wa kaumu hiyo walieneza ibada ya kuabudu masanamu. Baada ya Waislamu kusimamisha dola ya Kiislamu mjini Madina, ukoo huo wa Bani Mustaliq ambao uliendelea kuabudu masanamu, ulitangaza utayarifu wake kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Kwa sababu hiyo Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na kundi la wafuasi wake, alilazimika kupambana na kaumu hiyo na hatimaye kuishinda vibaya.

Katika siku kama ya leo miaka 301 iliyopita, Peter the Great, mfalme wa tatu wa Urusi kutoka katika familia ya Romanov aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 53. Alizaliwa 1696 na alifanikiwa kushika hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia Ivan Alexeyevich. Aliamini kwamba upatikanaji wa maji ya moto ungeifanya Urusi kuwa nguvu ya kibiashara na baharini duniani. Kwa hivyo, alielekeza juhudi zake kwenye pwani za Bahari za Baltiki na Bahari Nyeusi. Petr the Great pia alijaribu kusonga mbele hadi Ulaya kupitia eneo la Milki ya ufalme wa Othmania na nchi za Poland na Sweden, na akafanikiwa kiasi. Peter the Great alikuwa mtu katili na ambaye hakuacha kufanya chochote ili kufikia malengo yake, na kwa sababu hii, wakati wa utawala wake, maisha ya watu, mali, na uhuru wao hayakuwa salama kutokana na uvamizi wake.

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Peter Kropotkin, mwanafalsafa na mwanajiografia wa Urusi. Alizaliwa mwaka 1842 katika familia ya watu mashuhuri huko Moscow. Kropotkin alijiunga na jeshi akiwa kijana, lakini baada ya muda alijiuzulu na kusoma katika Chuo Kikuu cha St. Petersburg. Alifanya utafiti wa kina wa kijiografia huko Siberia kaskazini mwa Urusi, na pia nchini Finland na Sweden. Mwanamapinduzi huyu wa Urusi alikamatwa na kufungwa nchini mwake mwaka 1874 kwa kuendesha harakati za kupinga serikali, lakini alitoroka miaka miwili baadaye na kwenda Ulaya.

Katika siku kama hii ya leo miaka 63 iliyopita Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa jeshi wa Chama cha Baath. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita wananchi wa Iran walifanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Iran na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano hadi kuuangusha utawala wa Shah. Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran waliandamana katika siku kama hii wakijibu wito wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliyewataka waiunge mkono serikali ya muda ya Mapinduzi. Katika upande mwingine maafisa na vikosi vya Jeshi la Anga la Iran waliokuwa katika sare zao za kijeshi, walielekea kwa Imam na kutangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu na uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini. Katika mazungumzo hayo, Imam Ruhullah Khomeini aliwaambia wanajeshi hao kwamba walikuwa watumishi wa utawala wa kitaghuti na sasa wamejiunga na Qur'ani. Hatua ya vikosi vya Jeshi la Anga la Iran ya kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini iliukasirisha sana utawala wa Shah.