Feb 12, 2026 02:30 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Sha'ban 1447 Hijria sawa na Februari 12 mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1143 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir, alimu na mwanamapambano mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw).

Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina, na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwaua na kuwabaidisha watu wa familia ya Mtume SAW akiwemo Imamu Hassan Askari (as), Ali Atroosh alipelekwa mjini Samarra, kaskazini mwa mji wa Baghdad, Iraq kwa amri ya watawala hao ikiwa ni baada ya baba yake kubaidishwa mjini hapo. Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh alijifunza elimu ya dini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa msomi mkubwa huku akitabahari pia katika uwanja wa mashairi.

Mbali na hayo alijihusisha na harakati za kisiasa ambapo katika kipindi cha mwamko wa Maalawi huko Tabarestan, kaskazini mwa Iran, Atroosh alikimbilia katika eneo hilo. Baada ya kuanguka utawala huo, aliufufua huku akitawala sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini mwa Iran kwa uadilifu na usawa, sambamba na kueneza mafundisho ya dini ya Mtume Muhammad (saw). Katika harakati zake alifanikiwa kuwaingiza maelfu ya watu katika dini ya Uislamu.

'Al-Bisat' 'Tafsir al-Atroosh' na 'Imamatul-Kabir' ni miongoni mwa makumi ya vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo. ***

Miaka 714 iliyopita na katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Hussein bin Abdullah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharafuddin, aliaga dunia.

Alikuwa mpokezi wa hadithi na na mwanafasihi mkubwa. Abdullah Tayyebi alibobea katika elimu za fasihi ya lugha ya Kiarabu na alihesabiwa kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika zama zake. Mwanazuoni huyo alikuwa akitilia mkazo suala la kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na Hadithi.

Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni 'Tafsirul-Qur'an' na 'Sherh al Meshkat'.     ****

Miaka 630 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Nuruddin Abdul-Rahman Jami, mshairi na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya 9 Hijria.

Alizaliwa katika mji wa Jam ulioko katika mkoa wa Khorasan kaskazini mashariki mwa Iran. Alianza kujifunza elimu mbalimbali akiwa katika rika la ujana. Alikuwa na mapenzi na itikadi thabiti na watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW na katu hakuwahi kuwasifu wafalme na watawala.

Silsilat al-Dhahab na Baharestan ni baadhi ya athari za Nuruddin Abdul Rahaman Jami.    *** 

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, alifariki dunia Immanuel Kant, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Ujerumani, akiwa na umri wa miaka 80.

Kant alizaliwa mwaka 1724 katika familia ya kidini na alitumia sehemu kubwa ya umri wake katika kusoma, kufundisha na kuandika vitabu katika taaluma mbalimbali kama hisabati, nujumu, mantiki na falsafa.

Ameacha athari nyingi ikiwa ni pamoja na 'Misingi ya Falsafa' 'Ukosoaji wa Akili ya Kivitendo' na 'Ukosoaji wa Akili ya Nadharia.'   ****

Siku kama ya leo miaka 217 iliyopita alizaliwa mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza, Charles Darwin.

Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu namna ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kisayansi. Baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species".

Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa.    ****

Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita nchi ya Chile ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Chile ilikaliwa kwa mabavu na Uhispania mnamo mwaka 1536.

Mwaka 1788, Mfalme Charles III aliyekuwa mfalme wa Uhispania aliangalia upya makoloni yake na hivyo akaamua kuikabidhi nchi hiyo kwa Peru. Harakati ya kwanza ya kupigania uhuru nchini Chile ilianza mwaka 1814 Miladia. Katika harakati hizo wapiganaji waliokuwa wanataka kujitenga walishindwa vibaya na askari wa serikali ya kikoloni.

Hata hivyo mwaka 1817, José de San Martín, raia wa Argentina akishirikiana na maelfu ya wapiganaji alianzisha harakati dhidi ya makoloni ya Mfaransa ikiwemo Peru na Chile. Kwa uungaji mkono wa raia wa Chile hatimaye alifanikiwa kuwatimua wakoloni wa Uhispania na nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 1818 Miladia.     ***

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita aliuawa shahidi mwasisi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na mwanamapambano mashuhuri wa Misri, Ustadh Hassan al Banna.

Hassan al Banna aliuawa shahidi katika njama iliyopangwa na Uingereza kwa kushirikiana na Mfalme Faruq wa Misri. Alianza mapambano yake dhidi ya ukoloni na vibaraka wake akiwa chuo kikuu ambapo alianzisha harakati ya kupambana na sera za kupinga dini ya Kiislamu za Uingereza kwa kuasisi hatakati ya Ikhwanul Muslimin hapo mwaka 1928. Harakati hiyo ilikuwa kwa kasi na kuenea katika nchi za Syria, Jordan, Lebanon, Palestina na katika baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika.

Serikali ya Misri ilipiga marufuku harakati ya Ikhwanul Muslimin mwaka 1948 na kuwatia jela wanachama wake wengi na kisha kumuua shahidi kiongozi wake Sheikh Al Banna.      ****

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.

Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah.

Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.    ****

Tarehe 12 Februari miaka 18 iliyopita aliuawa shahidi Imad Mughnia maarufu kwa jina la Haj Ridhwan, ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa Hizbullah ya Lebanon, katika shambulizi la kigaidi lililofanyika mjini Damascus, Syria.

Kamanda Mughnia aliuawa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa na vibaraka wa Israel katika gari lake. Shahid Mughnia alijiunga na harakati za mapambano baada ya uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Baadaye kidogo alijiunga na harakati ya Hizbullah na kushika nyadhifa za juu katika harakati hiyo.

Shahidi Mughnia alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Hizbullah dhidi ya Israel katika vita vya siku 33 vya utawala huo nchini Lebanon mwaka 2006.   ***