Jumamosi, 14 Februari, 2026
Leo ni Jumamosi 25 Shaaban 1447 Hijria mwafaka na 14 Februari 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1310 iliyopita, aliuawa kamanda wa Kiiran, Abu Muslim Khorasani, kwa amri ya Mansur, aliyekuwa mtawala wa wakati huo wa Bani Abbasi. Abu Muslim Khorasani alikuwa kiongozi wa harakati liyopewa jina la 'Siah Jamegan' huko Khorasan ambayo ilianzisha uasi dhidi ya mtawala dhalimu wa Bani Umayyah. Katika kipindi kifupi watu wengi wa vijiji na miji mingi ya Khorasan walijiunga na kundi hilo. Baada ya vita vingi Abu Muslim na wafuasi wake walifanikiwa kuwashinda watawala hao wa Bani Umayyah. Kwa utaratibu huo kuliandaliwa uwanja wa kuhitimisha kabisa utawala wa Bani Umayyah na kuingia madarakani watawala wa Bani Abbas. Katika kipindi hicho Abu Muslim Khorasani alikuwa na nafasi kubwa kiasi cha kumfanya Mansur, mtawala wa ukoo wa Bani Abbas kujawa na hofu kubwa. Kwa sababu hiyo alipanga njama ya kumuua. Baada ya mauaji hayo wafuasi wa Abu Muslim Khurasani walianzisha mapambano na kulipiza kisasi cha damu yake na mapimbano hayo yaliendelea kwa muda mrefu.
Miaka 88 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni waliokuwa na silaha na wanachama wa kundi la kigaidi la Palmach waliendeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Palestina kwa kutekeleza shambulizi la kigaidi dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sa'sa' huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika operesheni hiyo iliyoendelea hadi kesho yake nyumba 20 za raia wa Palestina ziliharibiwa na watu 60 waliokuwemo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wakauawa kwa umati.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita sawa na tarehe 14 Februari mwaka 1945, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia nchi mbili za Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya Ujerumani. Ndege 1773 za kijeshi zilitumiwa katika mashambulizi hayo ambayo ndiyo yaliyokuwa na hasara kubwa zaidi ya mali na nafsi duniani hadi hii leo. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Marekani na Uingereza yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tatu yalisawazisha na ardhi miji kadhaa ya viwanda ya Ujerumani na kuifanya majivu matupu. Raia kati ya laki moja na nusu hadi laki mbili na nusu waliuawa kinyama katika mashambulizi hayo.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini alitoa fatuwa iliyomtambua Salman Rushdie, mwandishi wa kitabu cha "Aya za Shetani" au Satanic Verses kuwa ameritadi na kutoka katika dini ya Kiislamu. Katika kitabu hicho Rushdie alimvunjia heshima na kudhalilisha Mtume Muhammad (saw), kitabu kitukufu cha Qur'ani na matukufu mengine ya Kiislamu. Uandishi na uchapishaji wa kitabu hicho ulifanyika kwa njama na msaada wa nchi za Magharibi. Hata hivyo fatuwa ya Imam Khomeini dhidi ya murtadi Salman Rushdie, iliwaamsha Waislamu na kuwatahadharisha kuhusu njama hiyo. Fat'wa hiyo ya Imam Khomeini iliungwa mkono na waandishi wengi huru duniani, maulamaa wa Kiislamu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
Katika siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, aliuawa Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon kwenye mlipuko wa bomu lililotegwa garini huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Hariri alikuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri nchini Lebanon na wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa miaka 61. Hariri alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Lebanon kutokea mwaka 1992, muda mfupi baada ya kumalizika vita vya ndani vya Lebanon hadi mwaka 1998, na kuchukua tena wadhifa huo mwaka 2000 hadi 2004.