Jumapili, 15 Februari, 2026
Leo ni Jumapili 26 Shaaban 1447 Hijria mwafaka na 15 Februari 2026 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 1342 iliyopita aliaga dunia Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa Bani Umayya. Aliingia madarakani akiwa Khalifa 101 Hijria, baada ya Omar bin Abdul-Aziz. Alikuwa mlevi na mpenda starehe na hakuwa akizingatia kabisa ya Kiislamu. Kutokana na kuwa alikuwa jamaa wa Hajjaj bin Yusuf Thaqafi, aliwateua watu wengi kutoka katika familia hiyo kwa ajili ya kushikilia nyadhifa mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 462 iliyopita, alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei.Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Mwislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Miaka 244 iliyopita katika siku kama ya leo, vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi saba, vilikuwa ni mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo, na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi.
Katika siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, Alfred North Whitehead mwanahisabati mahiri wa Uingereza alizaliwa. Baada ya kukamilisha masomo yake alianza kufundisha falsafa na hisabati katika vyuo vikuu vya Marekani na Uingereza. Alfred North Whitehead ameandikka pia vitabu kuhusiana na hisabati. Tofauti na ilivyokuwa katika zama zake za ujana ambapo alikuwa na mapenzi makubwa na hisabati, katika miaka ya mwisho wa umri wake aliondokea kuwa na mapenzi na falsafa. Kutokana na kuwa Alfred North Whitehead aliondokea katika familia ya kidini, alikuwa akitoa umuhimu upande wa kimaanawi wa dunia kuliko upande wa kimaada.
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka kumi. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na muqawama wa mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa ni kuizatiti na kuitia nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyatoa majeshi ya Urusi katika ardhi yao.