Feb 16, 2026 03:01 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumatatu 27 Sha'ban 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 16 Februari 2026.

Miaka 181 iliyopita katika siku kama ya leo aliuawa Sayyid Ali Muhammad Shirazi aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya “Bab” ambaye alidai kuwa ndiye Imam Mahdi (AF) na baadaye akadai kuwa ni Mtume.

Alizaliwa mwaka 1235 Hijria Qamariya katika mji wa Shiraz nchini Iran na alionekana kuwa na itikadi potofu akiwa bado shuleni. Muhammad Ali Bab, ambaye hakuwa na elimu ya juu, alifuatwa na watu majahili na kuungwa mkono na wakoloni.

Baada ya kudai kuwa ndiye Imam wa mwisho katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw), yaani Imam Mahdi (AF), Bab alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba dini ya Uislamu imefutwa. Wanazuoni wa zama hizo walifichua urongo wake na kumchukulia hatua. Hata hivyo aliendelea kulingania itikadi zake potofu, na katika siku kama ya leo Amir Kabiir aliyekuwa kiongozi wa zama za Qajar alitoa amri ya kunyongwa kwake.

Kundi la "Babiyya" na baadhi ya makundi mengine yenye potofu yaliibuka wakati wa ushawishi wa wakoloni wa Uingereza na Urusi katika nchi za Kiislamu, kwa lengo la kudhoofisha imani za kidini za watu na kuzusha hitilafu miongoni mwa Waislamu.***

Katika siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917. 

Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo.

Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.    *****

Siku kama leo miaka 80 iliyopita, inayosadifiana na 16 Februari 1946, kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa.

Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu ambazo ni wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia.

Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwa na malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto, hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa.  ****

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, Aliaga dunia Ayatullah Sheikh Abdul-Hussein Rashti, fakihi na mwanafalsafa wa Kiirani.

Alizaliwa mwaka 1292 Hijria katika mji wa Karbala, Iraq.  Akiwa pamoja na baba yake alielekea Rasht Iran akkiwa bado kijana mdogo na kusoma masomo ya msingi na ya kati katika mji huo.

Akiwa na umri wa miaka 20 Abdul-Hussein Rashti alielekea Tehran na kuhudhuria masomo na darsa za wanazuoni wakubwa katika zzama hizo kkama Sheikh Muhammad Hassan Ashtiyani, Sheikh Ali Nuri, Sayyid Shahab al-Din Tabrizi Shirazi na Mirza Abul-Hassan.   *****

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Bahman, idadi kadhaa ya viongozi wa utawala wa Kipahlavi walinyongwa baada ya kupatikana na hatia ya usaliti na kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Iran.

Licha ya kuwa kwa mtazamo wa wananchi Waislamu wa Iran jinai za viongozi hao wa utawala dhalimu wa Shah zilikuwa wazi na bayana, lakini kwa amri ya Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu kuliundwa Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na kushughulikia kesi za viongozi hao waliokuwa wametiwa mbaroni na vikosi vya wananchi. Katika kesi ya kwanza, makamanda wanne wa jeshi ambao walikuwa na mchango mkubwa katika mauaji dhidi ya raia walihukumiwa kunyonga.

Mmoja wa watu hao alikuwa Nematollah Nasiri, Mkuu wa Shirika la Intelijensia na Usalama la Shah lililokuwa maarufu kama SAVAK, ambye alikuwa mkuu wa shirika hilo la kuogofya kwa zaidi ya miaka 13 ambapo katikak kipindi ckae cha uongozi aliwatia mbaroni maelefu ya wanamapambano wa kiislamu, kuwatesa na kuwaua wengi miongoni mwao.    ******

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, sawa na tarehe 16 Februari 1984, Sheikh Raghib Harb, Imam wa Swala ya Ijumaa katika kijiji cha Jibshit cha kusini mwa Lebanon na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon dhidi ya utawala ghasibu wa Israel aliuawa shahidi na askari wa utawala huo vamizi.

Sheikh Raghib alikuwa mmoja wa wanazuoni wanamapambano amilifu kusini mwa Lebanon kabla ya kuuawa kwake shahidi aliwahi kutiwa mbaroni na makachero wa Wazayuni wavamizi kutokana na mapambano na wito wake wa kuwataka wananchi wasimame na kupambana na Wazayuni.

Wakati wa kuzikwa mwili wa shahidi Sheikh Raghib Harb, kulitokea mapigano makali baina ya vijana wa kitongoji cha Jibshit na wanajeshi wa Israel ambayo yalipelekea kuuawa na kujeruhiwa idadi kadhaa ya Waislamu madhulumu wa Lebanon.    ****

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa nchi hiyo.

Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon.

Hujuma hiyo ilizusha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu kwamba hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon. ***