Jumanne, 17 Februari, 2026
Leo ni Jumanne 28 Sha'ban 1447 Hijria sawa na 17 Februari 2026.
Katika siku kama ya leo miaka 817 iliyopita alifariki dunia Ibn Hajib, mtaalamu wa Hadithi na mwanahistoria maarufu wa Kiislamu.
Ibn Hajib alizaliwa mwaka 593 Hijiria huko Damascus, Syria na kuelekea kwenye miji tofauti kwa ajili ya kusoma elimu ya Hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa wakati huo.
Alitambuliwa kuwa gwiji wa elimu ya Hadithi katika zama zake kutokana na umahiri wake mkubwa katika taaluma hiyo. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa. ***
Siku kama ya leo miaka 217 iliyopita, vilimalizika vita vya umwagaji damu vya Zaragoza vilivyopiganwa kati ya wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Uhispania.
Ufaransa ilipata ushindi katika vita hivyo na kuukalia kwa mabavu mji wa Zaragoza ulioko mashariki mwa Uhispania. Vita hivyo vilianza Novemba 15 mwaka 1808, kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon. ***
Katika siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, aliaga dunia Johann Heinrich Pestalozzi, msomi wa Uswisi na mmoja wa walimu mashuhuri.
Pestalozzi alikuwa mjuzi wa elimu nyingi hasa hisabati na tiba na alizungumza lugha kadhaa za kimataifa.
Msomi huyo wa Uswisi alikuwa na mtindo wake makhsusi wa kufundishia ambapo aliweza kutoa mafunzo ya masuala mbalimbali kwa watoto kwa wakati mmoja. ***
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Iran na utawala wa Baath wa Iraq yalianza huko New York nchini Marekani.
Katika hali ambayo mazungumzo hayo hayakuwa na natija ya maana na hata kulikuwa na uwezekano wa kuvunjika kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imethibitisha nia yake njema kwa jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa hususan Katibu Mkuu wake. ****
Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, mkataba wa kuasisiwa Jumuiya ya Magharibi ya Kiarabu za ulitiwa saini huko Morocco kwa kuhudhuriwa na Marais wa nchi za kaskazini mwa Afrika.
Nchi washiriki wa mkataba huo zilikuwa Libya, Mauritania, Algeria, Tunisia na mwenyeji Morocco. Lengo la kuasisiwa jumuiya hiyo lilikuwa kuanzisha taasisi ya kieneo kwa lengo la kupanua ushirikiano baina ya nchi wanachama na kupunguza utegemezi kwa nchi za Magharibi.
Hata hivyo, hitilafu za kimitazamo za baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Magharibi ya Kiarabu kama Algeria na Morocco kuhusiana na suala la Sahara Magharibi na vilevile mizozo ya mipaka na kisiasa zilizuia kufikiwa malengo ya kuasisiwa jumuiya hiyo. ***
Tarehe 17 Februari miaka 15 iliyopita ilianza harakati ya wananchi wa Libya dhidi ya utawala wa kidikteta wa Kanali Mummar Gadafi.
Libya ilikuwa nchi ya tatu kukumbwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu na kuziangusha tawala kadhaa za kidikteta. Baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Zainul Abidin bin Ali nchini Tunisia na ile wa dikteta wa zamani wa Misri, Husni Mubarak, wananchi wa Libya pia walianzisha harakati kubwa dhidi ya dikteta wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.
Awali Gaddafi alidhani kwamba angeweza kuzima harakati hiyo ya wananchi kwa kutumia jeshi na vyombo vya usalama na kwa msingi huo alianza kutumia mkono wa chuma na kuua wananchi waliokuwa wakiandamana. Wanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO pia walipanda mawimbi ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na kushambulia vituo vya kijeshi na viwanda vya Libya.
Hatimaye Muammar Gaddafi aliyeitawala Libya kwa kipindi cha miongoni minne kwa mkono wa chuma aliondolewa madarakani kwa madhila na kuuawa kwa kudhalilishwa na kisha akazikwa sehemu isiyojulikana. **
Siku siku kama ya leo miaka 10 iliyopita Mohamed Hassanein Heikal mwandishi na mwanafikra mtajika wa Misri alifariki dunia.
Mohamed Heikal alizaliwa Septemba 23, 1923 katika jimbo la Qalyubia huko Misri. Alikuwa mhariri mkuu katika gazeti la al-Ahram la Misri kwa muda wa miaka 17. Heikal alikuwa muasisi wa kituo mashuhuri cha utafiti wa kisiasa na kiistratejia cha al-Ahram. ****