May 28, 2026 04:33 UTC
  • Alkhamisi tarehe 28 Mei , 2026

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhulhijja 1447 Hijria mwafaka na tarehe 28 Mei 2026.

Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, alifariki dunia Eugène Burnouf, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufaransa. Burnouf alizaliwa Paris mwaka 1801 na kuhitimu somo la sheria. Hata hivyo hamu yake kubwa ya kusomea lugha na fasihi sambamba na kuvutiwa na masuala ya Mashariki ya Kati, vilimfanya ajifunze lugha za Sanskrit na Iran ya kale. Eugène Burnouf pia alijifunza utamaduni wa nchi za Iran na India. Miongoni mwa kazi zilizozifanya msomi huyo ni pamoja na kufasiri sehemu za kitabu cha Avesta. Vitabu vya ‘Dondoo za Yasna’ ‘Historia ya dini ya Mabudha’ na ‘Babr Bayan’ ni miongoni mwa vitabu vya Eugène Burnouf.  ***

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1940, Ubelgiji ambayo ilitangaza kutoegemea upande wowote mwanzoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ilitekwa na majeshi ya Kinazi ya Ujerumani.

Majeshi ya Ubelgiji ambayo yalikuwa yakipata usaidizi wa Uingereza, yalisimamisha vita kutokana na amri ya Mfalme Leopold wa Tatu, licha ya kusimama kidete kwa muda wa siku 18 dhidi ya majeshi ya Kinazi ya Ujerumani.

Hatua hiyo ya Mfalme Leopold, iliwakasirisha mno wananchi wa Ubelgiji na kuandaa mazingira ya kuondolewa kwake madarakani hapo mwaka 1951.  ***

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1964, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliafikiana na fikra ya kubuniwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ambapo mwanzoni ilizijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha.

Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 likaanzisha shughuli za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974 PLO ilikubaliwa kuwa manachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa ambapo kufikia mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia.

Taratibu PLO ilianza kupoteza muelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo kufikia mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, ilikubali kuutambua rasmi utawala huo kwa kutia saini mapatano ya Oslo.   ***

Tarehe 7 Khordad miaka 46 iliyopita kwa mujibu wa mwaka wa Hijria Shamsia lilifunguliwa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kislamu).

Ufunguzi wa muhula wa kwanza wa bunge la kutunga sheria katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatambuliwa kuwa hatua muhimu na siku hii najulikana hapa nchini kama "Siku ya Sheria".

Jukumu la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni kutunga sheria na kusimamia moja kwa moja utendaji wa Rais na serikali. Idadi ya wajumbe wa Bunge la Iran ni 290 na wanachaguliwa kwa kura za moja kwa moja za wananchi.

Wafuasi wa dini ndogo zinazotambuliwa rasmi nchini Iran, ingawa wengi wao hawajatimiza akidi inayohitajika ya watu 150,000, wanawakilishwa pia bungeni. Ripoti kamili ya mijadala ya umma ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inatangazwa moja kwa moja kwenye redio ya taifa, na vyombo vya habari na magazeti rasmi pia huchapisha maudhui yake.   *****

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita sawa na tarehe 28 Mei 1991, utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi.

Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 Milaadia wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa.

Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili, shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1930 hadi 1974 na kisha akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.   ***

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Mei 1998, kwa mara ya kwanza Pakistan ilifanya majaribio matano ya makombora ya nyuklia.

Majaribio hayo yalifanyika zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu hasimu wake, yaani India, ifanye majaribio ya kombora la nyuklia. Baada ya hapo nchi hizo mbili zimekuwa zikifanya kwa zamu majaribio yao ya makombora ya nyuklia.

Majaribio ya nyuklia ya Pakistan, kinyume na yale yanayofanywa na India, yamekuwa yakizikasirisha mno nchi za Magharibi za Marekani na Ulaya, na kufikia hatua ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.   ***