Jumamosi, Juni 6, 2026
Leo ni Jumamosi 20 Mfunguo Tatu Dhulhija 1447 Hijria mwafaka na 6 Juni 2026.
Miaka 1319 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Imam Musa Kadhim AS, mmoja wa wajukuu vipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Mpaka anatimiza umri wa miaka 20, mtukufu huyo alikuwa pamoja na baba yake mpenzi Imam Jaafar Sadiq AS akichota maarifa kwenye bahari ya elimu kubwa. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Musa Kadhim AS alibeba jukumu la Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo katika kipindi chote hicho alihimili na kuvumilia tabu na misukosuko mingi.
Miaka ya mwanzoni ya Uimamu wa Imam Musa Kadhim, ilisadifiana na kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kushika hatamu za utawala wa Bani Abbas.
Imam Musa Kadhim AS alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kusomesha na kulea watu kimaadili na kuwaelimisha juu ya utamaduni na mafundisho sahihi ya Uislamu. Lakini kutokana na kumhisi ni hatari kwake, utawala wa Bani Abbas ulimuweka gerezani mtukufu huyo ili kuwafanya watu wakose nuru ya uongofu na elimu ya Imamu huyo mwema na kubaki kwenye giza la ujinga na ujahili.
Imam Musa Kadhim AS alikuwa alimu mkubwa zaidi na mja mwema na mkarimu zaidi kuliko watu wote wa zama zake. Alipambika kwa khulka njema, huruma na ukarimu usio na kifani na alikuwa maarufu mbele ya watu wote kwa utukufu wa nafsi, ukarimu, moyo wa kutoa kwa siri na kwa dhahiri na kuwasamehe wanaomkosea.
Mbali na kutoa mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imamu huyu muadhamu, nakunukulieni maneno mazuri na ya hekima ya mtukufu huyo aliposema: “Njia bora inayomkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu baada ya kumjua Yeye Mola ni Sala, kuwatendea wema wazazi na kuacha uhasidi na kujiona”. ***
Siku kama ya leo, miaka 227 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow.
Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake.
Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru. ***
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Lebanon.
Katika uvamizi huo, jeshi la Israel liliuvamia na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bairut. Aidha askari hao wa utawala haramu wa Kizayuni, waliharibu miundombinu, viwanda na viunga vya mji huo, sanjari na kutekeleza jinai mbalimbali dhidi ya wakazi wake.
Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa Wazayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Mwezi Septemba mwaka huo huo, jeshi hilo lifanya mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika kambi mbili za Sabra na Shatila karibu na mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 2000, kufuatia ushindi wa wanamapamgano wa Hizbullah, wanajeshi vamizi wa Israel walilazimika kuondoka kwa madhila katika maeneo yote ya Lebanon waliyokuwa wameyakalia kwa mabavu. ***
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Juni 1984, jeshi la India lilishambulia hekalu kubwa la Masingasinga lililojulikana kama Hekalu la Dhahabu katika mjini wa Amritsar makao makuu ya jimbo la Punjab, magharibi mwa India na kuua waasi wa Kisingasinga wasiopungua 1,000.
Serikali ya India ilidai kuwa shambulio hilo lilifanywa baada ya kupatikana habari za kufichwa silaha nyingi kwenye hekalu hilo, kwa shabaha ya kuanzisha uasi na mashambulizi dhidi ya serikali kuu.
Masingasinga hao nao walilipiza kisasi kwa kumuuwa Indira Ghandi, Waziri Mkuu wa India mwaka huohuo, kiongozi ambaye ndiye aliyetoa amri ya kushambuliwa hekalu hilo. ***
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Juni, mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliokuwa na huzuni kubwa waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Kiislamu, ya Behesht Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran.
Zaidi ya watu milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomeini, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye walielekea eneo la Behesht Zahra kwa ajili ya mazishi.