Jun 27, 2026 03:29 UTC
  • Jumamosi 27 Juni 2026

Leo ni Jumamosi 12 Mfunguuo Nne Muharram 1448 Hijria mwafaka na 27 Juni 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zaynab (as) walitekeleza majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu.

***

Siku kama ya leo miaka 1353 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.   

***

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita inayosadifiana na 27 Juni 1977, nchi ya Djibouti iliyoko karibu na eneo la Pembe ya Afrika ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa baada ya kupita miaka kadhaa ya harakati ya kupigania uhuru. Tokea mwaka 1896 nchi hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Somalia Ufaransa na kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini baada ya kupita miongo minane, hatimaye nchi hiyo ilipata uhuru. Djibouti ilikuwa nchi ya mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na inahesabiwa kuwa nchi muhimu katika eneo la kiistratijia kwa kuwa inapakana na Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, kwenye eneo la lango bahari la 'Bab Mandab'. 

***

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Ayatullah Khamenei, Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye wakati huo alikuwa mwakilishi wa Imam Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na Imam wa Ijumaa wa Tehran, alinusurika kifo katika jaribio la mauaji lililofanywa na mawakala wa kundi la kigaidi la Mojahedin-e Khalq (MEK). Shambulio la magaidi hao lilimjeruhi vibaya Ayatullah Khamenei kwa kulipua bomu alipokuwa akitoa khutba katika mojawapo ya misikiti ya Tehran.

***

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani aliyekuwa mrithi wa Amir wa Qatar alifanya mapinduzi dhidi ya baba yake. Sheikh Hamad alimuondoa madarakani baba yake, Sheikh Khalifa bin Hamad Aal Thani wakati Amiri huyo wa zamani wa Qatar alipokuwa safarini nchini Uswisi. Sheikh Khalifa ambaye alikuwa kiongozi wa Qatar tangu mwaka 1972 alifanya jitihada kubwa za kurejea madarakani lakini hakufanikiwa. Nchi ndogo ya Qatar iko kusini mwa Ghuba ya Uajemi na inapakana na Saudi Arabia. Nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.