Oct 02, 2016 02:45 UTC
  • Jumapili, Oktoba 2, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 30 Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah mwaka 1437 Hijiria, mwafaka na Oktoba Pili, 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, alizaliwa Mahatma Gandhi, kiongozi wa harakati ya kupigania uhuru nchini India katika moja ya vijiji vya jimbo la Gujarat. Mwaka 1891 Miladia Gandhi alirejea kutoka nchini Uingereza na kuishi mjini Mumbai. Mwaka 1893 Miladia Mahatma Gandhi alielekea mjini KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini. Akiwa nchini humo alishuhudia ubaguzi wa rangi wa jamii ya wachache ndani ya taifa hilo. Mwaka 1917 Miladia na baada ya kurejea nchini kwake alipata umashuhuri mkubwa. Na miaka michache baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia yaani akiwa na umri wa miaka 33 aliongoza mapambano kwa ajili ya kuwaokoa watu wake sanjari na kupigania uhuru wa India kutoka mikononi mwa Waingereza ambapo hatimaye na baada ya kuvumilia matatizo mengi akiwa na shakhsia tofauti kama vile Jawaharlal Nehru akafanikiwa kulipatia uhuru taifa hilo hapo mwaka 1947 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1904, alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Siku zote mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi ambapo baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita yaani sawa na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na ilipoanza karne ya 19, Wafaransa wakawa na satua zaidi nchini humo na ulipotimia mwaka 1849, nchi hiyo ikakoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Imam Khomein Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alielekea nchini Kuwait akitokea Iraq, baada ya serikali ya wakati huo ya Saddam Hussein kumzuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kimadhehebu, ili kwa njia hiyo utawala huo uweze kuhitimisha mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa wakati huo wa Shah nchini hapa. Hata hivyo na kwa lengo la kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran serikali ya Kuwait ilimzuia Imam Khomein kuingia chini humo, suala ambalo lilimlazimu shakhsia huyo kuelekea nchini Ufaransa. Miamala mibaya ya utawala wa Saddam dhidi ya Imam Khomein (MA), iliibua hasira kali za wananchi wa taifa la Iran wakati huo.

 

 

 

Tags