Jan 26, 2017 04:31 UTC
  • Jumatano 25 Januari, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 26 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 25, 2017.

Siku kama ya leo, miaka 11 iliyopia, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina ‘HAMAS’ ilipata ushindi muhimu katika uchaguzi wa Bunge la Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Katika uchaguzi huo ambao ulihudhuriwa na wasimamizi kutoka nje, na licha ya propaganda chafu za madola ya Kimagharibi na vyombo vya utawala wa Kizayuni wa Israel, HAMAS iliweza kushinda viti 76 kati ya viti vyote 132 vya Bunge na hivyo kuongoza katika uchaguzi huo. Kwa utaratibu huo harakati hiyo ikamchagua Ismail Haniya kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, na ikatangaza kwamba ilikuwa na lengo la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuishirikisha Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO. Hata hivyo utawala haramu wa Kizayuni na madola ya Kimagharibi hususan Marekani sanjari na kutekeleza mashinikizo ya kiuchumi, kisiasa, kijeshi na propaganda kwa pamoja yalifanya njama kwa ushirikiano wa utawala wa Kizayuni wa kutoitambua serikali hiyo halali ya wananchi ya Palestina na hatimaye kuiangusha serikali hiyo.

 Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Ujerumani kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda sugu vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijajulikana na kuna idadi kubwa ya waathirika katika nchi mbalimbali duniani.

Gerhard Henrik Armauer Hansen

Katika siku kama ya leo miaka 561 iliyopita kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika jumba la makumbusho.

Kiwanda cha uchapishaji

Na katika siku kama ya leo miaka 973 iliyopita, Ainuz-Zaman Marvazi, mwanahisabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Marvi wa Khorasani ya kale mji ambao leo unapatikana nchini Turkimestani. Ainuz Zaman alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hisabati, falsafa na  fasihi; hata hivyo alikuwa na mapenzi makubwa na elimu ya tiba. Alimu huyo alikuwa akijishughulisha na kazi ya utabibu huko Marvazi. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na kuvirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa.

عین الزمان قطّان مروزی

 

 

Tags